UNDANI WA AJALI YA IRINGA LEO: BASI LAUA ZAIDI YA ABIRIA 40 BAADA YA KUANGUKIWA NA KONTENA - LEKULE

Breaking

11 Mar 2015

UNDANI WA AJALI YA IRINGA LEO: BASI LAUA ZAIDI YA ABIRIA 40 BAADA YA KUANGUKIWA NA KONTENA


Muonekano baada ya kutokea ajali hiyo leo saa 3.30 Jumatano katika kijiji cha Changarawe wilayani Mafinga mkoani Iringa baada ya basi la abiria la kampuni iitwayo Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Dar.


AJALI mbaya ya gari imetokea asubuhi ya leo saa 3.30 Jumatano katika kijiji cha Changarawe wilayani Mafinga mkoani Iringa baada ya basi la abiria la kampuni iitwayo Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Dar kuelekea Mbeya na kusababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia 41 na majeruhi 22.

Habari kutoka eneo la tukio, zinasema ajali hiyo ilitokea wakati lori hilo lililokuwa limepakia kontena, likiwa katika mwendo wa kasi, lilipojaribu kulikwepa shimo lililokuwa katikati ya barabara na lilipotaka kurudi upande wake, ndipo lilipogongana uso kwa uso na basi hilo, linalokadiriwa kuwa na zaidi ya abiria 50 ndani yake.

“Hili lori lilipogongana na basi, kontena lake likaliangukia basi kiasi kwamba abiria wote wamelaliwa, watu wengine wanadaiwa walirushwa katika korongo kufuatia kishindo cha mgongano.

Hali ya kuwaokoa maiti na majeruhi ni ngumu kwa sababu hakuna gesi ya kukatia vyumba hapa Mafinga,” alisema shuhuda mmoja wa ajali hiyo ambaye hakutaja jina lake.

Watu ni wengi eneo la tukio na miongoni mwa viongozi wa serikali ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Juma Masenza.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ramadhani Mungi ambaye pia yupo eneo la tukio hivi sasa, amewasiliana na LEKULE na kuahidi kutoa ushirikiano zaidi baadaye kwa vile hivi sasa hekaheka ni nyingi.

No comments: