Tafsiri ya Waraka wa Maaskofu 32 - LEKULE

Breaking

13 Mar 2015

Tafsiri ya Waraka wa Maaskofu 32

IMERIPOTIWA kwenye vyombo vya habari, kuwa Maaskofu 32 wa Kanisa Katoliki wametaka Tume ya Jaji oseph Warioba iheshimiwe'.

Ni habari kubwa, na kuna habari pia za matamko ya Maaskofu wa makanisa mengine yasiyo ya Kikatoliki kuhusiana na Katiba. Matamko yaliyotolewa kwenye majira ya Pasaka.

Binafsi nimeupitia ulioolezwa kuwa ni ' Ujumbe wa Kichungaji wa Pasaka 2014 kwa Waumini na Watu wote wenye Mapenzi Mema'.

Nachangia hapa kama mtu mwenye mapenzi mema. Kwamba naungana na Maaskofu wetu hawa 32 kwenye hoja yao ya msingi; kwamba Tume ya Warioba iheshimiwe, hivyo basi, mawazo ya wananchi pia yaheshimiwe.

Nyongeza hapa, ni kuwa hata mawazo ya wachache nayo yaheshimiwe, na kwamba wapewe uhuru wa kujenga hoja zao na hata kuwashawishi walio wengi wakubaliane na hoja zao. Hiyo ndiyo demokrasia.

Maaskofu wetu wametumia hekima nyingi kwenye andiko lao. Hawakuweka misimamo yao juu ya mfumo upi wa muungano au serikali wanaoutaka. Wameelezea tu wanachokiona na kushauri na labda kuelekeza, maana, nao ni wachungaji. Ni viongozi. Wamesisitiza umuhimu wa uwepo wa umoja wenye kupigiwa mfano. Lakini, wameonyesha pia haja ya kuwepo kwa mabadiliko au mageuzi ya kimsingi.

Naam, nchi yetu imetumia rasilimali fedha nyingi na hata rasilimali wakati mwingi kwa kuipa, muda na fedha nyingi, Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba chini ya Jaji Warioba.

Yumkini, si kila maoni yaliyotolewa yanampendeza kila mtu au kikundi cha watu. Lakini, kwa vile tumekubaliana kutumia njia hiyo katika kufikia maridhiano ya kupata Katiba mpya, basi, ni vema na ni busara tukawa tayari kuyakubali na kuyaishi hata yale ambayo hatukuyapenda. Ni kwa vile kuna wengine wengi wenye kuyataka.

Na wengine hao ni watu wenye kustahili kusikilizwa matakwa yao. Na kimsingi, kama Taifa, tunaweza kutumia mfumo wa Serikali moja, mbili au tatu, alimradi, maamuzi hayo yajengwe katika misingi ya majadiliano na maridhiano. Bila malengo ya kumpata mshindi na mshindwa. Hivyo basi, tukiondoa tofauti za kiitikadi, tutabaki kuwa wamoja, na kitakachoamuliwa kitakuwa ni ushindi wetu wote kama taifa.

Tuking'ang'ania kusimamia kwenye makundi yetu na vyama vyetu, na kimsingi tukitanguliza maslahi binafsi, ya makundi na vyama, basi, hatari iliyo mbele yetu ni kushindwa wote, kama alivyopata kutamka Rais Jakaya Kikwete.

Na Rasimu hii ya Katiba, ukiacha hayo ya mifumo ya muungano na serikali, ina mengi mengine yanayotokana na mawazo ya wananchi wenyewe.

Mchakato huu umekuwa ni zaidi ya kupata Katiba mpya, kwa Watanzania wengi, umetoa fursa ya kupata ' elimu ya bure' juu ya somo la uraia. Kwamba kupitia mchakato huu wengi wamepata uelewa wa mambo mengi kuhusu nchi yao ambayo huko nyuma hawakuyajua. Si kuyapata tu, kwamba ni Watanzania wenyewe waliochangia kwenye maarifa haya mapya.

Kwa kuusoma waraka wa Maaskofu, na kwa kufuatilia mijadala hii ya sasa, jambo moja ni dhahiri, wananchi wengi, wa Bara na Visiwani, wanataka kuendelea na Muungano wao. Lakini, kuna waliyoyapendekeza ili kuimarisha Umoja na Ushirikiano wao. Maoni yao yasipuuzwe.

Na hakika, katika kipindi hiki tumeshuhudia kizungumkuti kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Na sasa tunamwona Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta akifanya jitihada za makusudi kuhakikisha Bunge hili linaendelea, ni katika kutafuta namna ya wenye kupingana wanafikia maridhiano ya namna ya kwenda mbele.

Na hilo haswa ndilo jukumu la spika kama mwenyekiti wa kikao cha bunge. Maana, hata ukisoma historia ya mabunge tangu karne ya 17, na kwa kuiangalia Uingereza, unaona kuwa spika alikuwa na jukumu kuu la kuwakilisha haki za wabunge dhidi ya korona (crown) ikiwa na maana ya mamlaka ya kifalme. Na utaratibu huo umeendelea na imekuwa sehemu ya tamaduni za kibunge.

Kwamba spika analiendesha bunge kwa kufuata kanuni. Kwamba hana upande, kwa Waingereza, hata kama spika ni mbunge, hapaswi kusimama na kulisemea jimbo lake la uchaguzi.

Wajibu wa spika pia ni kulinda haki za makundi yote ndani ya bunge, na hususan, haki za wachache. Spika akiwa mwanamume ni sawa na ' baba wa wabunge' na akiwa mwanamke anakuwa ' mama wa wabunge'. Na mzazi hapaswi kubagua wala kumpendelea waziwazi mtoto miongoni mwa watoto wake. Wote ni wa kwake.

Tunapoliangalia  hili la Katiba yetu, kuna umuhimu wa kuwapo kwa ' mitazamo ya kikatiba' kwa wajumbe wa Bunge la Katiba. Inahusu kinachoitwa ' constitutional thought'. Kwamba kukosekana kwa 'constitutional thought' kwenyewe kunaweza kuyumbisha Bunge la Katiba.

Kwamba fikra za wabunge zilipaswa ziwe za ' kikatiba zaidi', na hivyo kutazama namna Katiba itakavyokuwa bila kujiangalia wao kwa sasa wamekaa vipi, maana, watakachofikiria kitakuwa cha sasa zaidi, na pengine kesho inayoishia 2015, wakati Katiba itakuwa ni ya kuishi kwa miaka ambayo hata wao na watoto wao hawatakuwapo duniani.

No comments: