Simba yatenga mamilioni kumrudisha Tambwe - LEKULE

Breaking

23 Mar 2015

Simba yatenga mamilioni kumrudisha Tambwe



HII sasa kali, siku chache baada ya mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe kuanza kuonyesha makali yake ya kuzifumania nyavu, uongozi wa Simba ambao ulimfungashia virago nyota huyo mwishoni mwa mwaka jana, unadaiwa kuwa umeanza mikakati ya kuhakikisha unamrudisha katika kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.

Uongozi huo wa Simba chini ya rais wake, Evans Aveva, ulimfungashia virago Tambwe baada ya kudai kuwa kiwango chake kimeshuka.Kutokana na hali hiyo, Yanga ilijitoa mhanga na kuzifumbia macho tuhuma hizo za Simba na ikamsajili Tambwe kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Hadi hivi sasa Tambwe ameshaifungia Yanga mabao manne katika mechi 11 za ligi alizoichezea lakini amefunga mabao matatu katika michezo mitatu ya kimataifa akiwa na Yanga.

Juzi, straika huyo alifunga moja ya mabao makali katika Ligi Kuu Bara msimu huu alipoiwezesha Yanga kujikita kileleni mwa msimamo kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Mgambo JKT ambayo awali iliifunga Simba siku chache zilizopita.Habari za kumanika kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa, kuna mipango ambayo inafanywa kwa sasa ili kuhakikisha wanamrejesha tena Tambwe katika kikosi hicho na klabu hiyo imetenga mamilioni ili kuhakikisha inamnasa.

Yanga ilimsajili Tambwe kwa dau la dola 15,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 28 na analipwa mshahara wa dola 2,000, sawa na Sh milioni 3.7 wakati Msimbazi alikuwa akilipwa dola 1,000 (Sh milioni 1.85).
Viongozi wa Simba wanahaha kuhakikisha wanamuongezea dau ili atue kwa ajili ya msimu ujao.

“Unaambiwa kwa sasa mipango inasukwa kimyakimya ili kuhakikisha Tambwe anarudi tena Simba. Viongozi wanachotaka ni kuona mshambuliaji huyo anavaa tena uzi wetu msimu ujao,” kilisema chanzo chetu cha kuaminika.

Taarifa za ndani kutoka Yanga nazo zinasema klabu hiyo imeshtukia mbio za kimyakimya za Simba kumtaka Tambwe, hivyo inataka kukaa naye chini kumuongezea dau.Championi Jumatatu lilizungumza na Tambwe juu ya hilo na yeye bila kuficha alisema: “Hata mimi mipango hiyo nimeisikia kuwa jamaa wanataka nirudi.

“Lakini kusema kweli hilo litakuwa ni jambo gumu kwani akili yangu yote hivi sasa nimeielekeza katika kuhakikisha ninaisaidia timu yangu ya Yanga kufanya vizuri.” Nyota huyo ndiye aliyekuwa mfungaji bora msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara akiwa na Simba, baada ya kufunga mabao 19.

Katika hatua nyingine, Tambwe amemtangazia vita Mrundi mwenzake Didier Kavumbagu, akimwambia kwamba amerejea katika vita ya ufungaji. Tambwe juzi aliifungia Yanga bao moja katika ushindi dhidi ya Mgambo na kufikisha mabao matano msimu huu. Kavumbagu ni kinara, ameshazifumania nyavu mara 10.

“Hivi sasa nina mabao matano, Kavumbagu ana 10, tofauti iliyopo kati yangu na yeye siyo kubwa sana, hivyo ninaweza kumshusha siku yoyote kwenye nafasi hiyo na ikiwezekana ni katika mechi zetu mbili zijazo,” alisema.

No comments: