Rais Kikwete Asubiriwa Kutia Saini Ili Watu Kumi Wanyongwe - LEKULE

Breaking

31 Mar 2015

Rais Kikwete Asubiriwa Kutia Saini Ili Watu Kumi Wanyongwe

Utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa watu 10 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa, kutokana na kuhusika katika mauaji ya watu wenye ulemavu (albino), unasubiri saini ya Rais Jakaya Kikwete.
 
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF).
 
Katika swali lake, Barwany, alitaka kufahamu ni lini utekelezaji wa hukumu ya kifo kwa watu 10, waliokwisha hukumiwa adhabu ya kifo na Mahakama kutokana na kuhusika na mauaji ya albino, itatekelezwa.
 
Silima, alisema kwa mujibu wa taratibu za kisheria, adhabu ya kifo inapotolewa, utekelezaji wake husubiri saini ya Rais. “Sijapata taarifa kama hukumu hizi tayari Rais ameziwekea saini ili zitekelezwe ila nitafuatilia ili Sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
 
Katika swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kufahamu hadi sasa kuna kesi ngapi za mauaji ya walemavu wa ngozi zilizokwishatolewa hukumu baada ya kufikishwa mahakamani na kesi ngapi bado zinasubiri huku na ni kwanini zimechelewa kutolewa maamuzi.
 
Waziri alisema kati ya mwaka 2006 na 2015, jumla ya matukio 56 ya uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa nchini na kati ya matukio hayo 41 yalihusisha vifo 43, matukio 13 yahusisha majeruhi na mawili ya kupotea watu hao albino.
 
Alisema kesi 46 kati ya matukio 56 zilifikishwa mahakamani na kesi 10 zenye watuhumiwa 12 zilitolewa hukumu ya kifo na kesi 10 badi ziko chini ya upelelezi. Aidha kesi 26 watuhumiwa wake waliachiwa huru kwa kukosa ushahidi.
 
Silima alisema pia kesi 10 bado zinaendelea kusikilizwa mahakamani na ziko katika hatua mbalimbali.
 
“Kuhusu kuchelewa kwa hukumu au upelelezi wa baadhi ya kesi, kunachangiwa na sababu mbalimbali kama vile matokeo ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kutoka mamlaka za uchunguzi na mashahidi kutopatikana kwa urahisi na wakati".
 
Katika swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Al- Shamaar Kwegyir (CCM), alitaka kujua Serikali imefikia wapi katika kumtafuta mtoto Pendo Emmanuel mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa Kwimba, aliyechukuliwa mikononi mwa mama yake mzazi na mpaka sasa hajulikani alipo.
 
Akijibu swali hilo, Silima alikiri kuwa mpaka sasa Polisi inamtafuta na katika upelelezi unaoendelea jumla ya watu 14 wanashikiliwa na kuhojiwa kwa kuhusika kwa namna moja ama nyingine na tukio hilo, akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo.
 
“Pendo alichukuliwa mikononi mwa mama yake, na hali hii ndio inayoongeza ugumu wa matukio haya kwa Serikali kuyapatia ufumbuzi, jambo la msingi tusiwaachie polisi pekee, jamii nayo ijihusishe kuwalinda na kuwaripoti wahusika,” alisema.
 
Alisema hata yeye matukio hayo yanamtoa machozi kwa kuwa inaonesha sasa Watanzania wameondokewa na utu wa ubinadamu, na ndio maana wanafanya ukatili na unyanyapaa dhidi ya jamii ya albino.

No comments: