Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa Shinyanga. - LEKULE

Breaking

4 Mar 2015

Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa Shinyanga.


Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bw. Ali Nasoro Rufunga kuomboleza vifo vya watu 38 huku wengine 82 wakijeruhiwa usiku wa kuamkia tarehe 4 Machi, 2015.

Tukio hilo lakusikitisha limetokea katika kata ya Mwakata iliyoko katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kufuatia mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali na kuathiri watu 3,500. Katika kata mwakata iliyoathiriwa zaidi, kaya 350 zimeathiriwa katika kijiji cha Makata wakati katika kijiji cha Ngumbi, kaya 100 zimeathirika. Katika kijiji cha Magung'hwa, kaya 50 zimeathiriwa.

Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa wana-Shinyanga pekee bali ni wa taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya watanzania kwa ujumla.

Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao. Aidha amewahakikishia wafiwa wote kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa taifa.

No comments: