Raia wa kigeni wadaiwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa vijiji - LEKULE

Breaking

17 Mar 2015

Raia wa kigeni wadaiwa kuchaguliwa kuwa wenyeviti wa vijiji

Dodoma.Wabunge wanaotoka mikoa ya mipakani wamelalamikia kuhusiana na watu wasio raia kupiga kura na kuchaguliwa katika chaguzi kinyume cha sheria.
Wabunge hao ni Mbunge wa Viti Maalum, Josephine Genzabuke na Ally Keisy wote wa CCM walihoji juu ya tatizo hilo bungeni leo.
Katika swali lake la msingi Genzabuke aliihoji serikali juu ya wakimbizi waliopiga kura katika baadhi ya maeneo mkoani Kigoma ikizingatiwa ulikuwa uchaguzi wa serikali za mitaa haukuwa na vitambulisho maalum kama vile kadi ya kupigia kura.
Swali lililoulizwa pia na Keissy ambaye alisema katika jimbo lake kuna wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambao wamechaguliwa wakati si raia wa Tanzania?
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa,  Aggrey Mwanri alisema serikali itakuwa tayari kushirikiana na mbunge ili kuchunguza suala hilo na kuchukua hatua ya kulipatia ufumbuzi.
Hata hivyo, alisema ni jukumu la viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa pamoja na wananchi kuwabaini watu ambao siyo raia au wakazi wa eneo husika na kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Alisema kwa mujibu wa kanuni kabla ya siku ya uchaguzi orodha ya wapiga kura walioandikishwa hubandikwa katika kituo cha kupigia kura ili kuwawezesha wananchi wa eneo husika kubaini watu wasiokuwa na sifa wakiwemo wakimbizi au wasio wakazi wa eneo hilo

No comments: