Nesi atekwa Dar, watekaji wataka Sh5 mil - LEKULE

Breaking

17 Mar 2015

Nesi atekwa Dar, watekaji wataka Sh5 mil


Dar es Salaam. Watu wasiojulikana wamemteka Muuguzi wa Hospitali ya Mwananyamala, Pili Amiri, huku wakitoa sharti la kupewa Sh5 milioni ili wamuache huru.

Pili, mwenye umri wa miaka 26, alitekwa akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mwananyamala Komakoma, saa tano asubuhi, Alhamisi wiki iliyopita na kuingizwa katika gari linalodaiwa kuwa ni la watekaji hao.

Akizungumzia tukio hilo, mjomba wa Pili, Rahim Kangile alisema watekaji hao baada ya kumteka walipiga simu kwa kutumia namba ya Pili wakidai kutumiwa kiasi hicho cha fedha.

“Waliposema wanataka Sh3 milioni, ili wamuache, tuliwatumia lakini hawakufanya hivyo hadi jana, wakasema tuwatumie tena Sh2 milioni, tumetuma leo(jana) lakini mpaka sasa hakuna chochote tulichofanikiwa,” alisema.

Kangile alisema watekaji hao walitoa vitisho kuwa endapo malipo hayo hayatafanyika basi watafanya jambo lolote baya kwa muuguzi huyo.

“Tulipoona wanatoa vitisho tuliwatumia hizo hela lakini hawajafanya chochote la kuonyesha watamuachia Pili,”alisema.

Alisema watekaji hao walitaka fedha zitumwe katika akaunti ya NMB ya Pili, jambo ambalo lilitekelezwa na baadaye ikabainika kuwa miamala kadhaa imefanywa kupitia mtandao wa ATM kutoka kwenye akaunti ya muuguzi huyo.

Akizungumzia iwapo Pili alikuwa na maadui, Kangile alisema hawana chembe ya shaka kama muuguzi huyo alikuwa na ugomvi na watu hadi kufikia hatua ya kumteka.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophiniasis Ngonyani alisema Pili hakutekwa akiwa mazingira ya hospitali, bali akiwa nyumbani kwake na kueleza kuwa wanafamilia wametakiwa kutoa kiasi hicho cha fedha ili aachiwe huru.

“Ni kweli huyu muuguzi wetu ametekwa tangu Alhamisi iliyopita, tumezipata taarifa kutoka kwa ndugu zake, baada ya kutokuonekana nyumbani kwa siku kadhaa,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa mjomba wa wanafamilia, siku moja baada ya watekaji kumteka msichana huyo, walipiga simu wakitaka kupewa kiasi cha Sh3 milioni.

Dk Ngonyani alisema polisi wameshapewa taarifa za tukio hilo na wanaendelea kufanya kazi yao ili kupata taarifa za ndani zaidi.

Kamanda wa Polisi, mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Camillius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mpaka sasa hawana uhakika kama ni utekaji au nesi huyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Wambura alisema polisi wanafanya uchunguzi kujua alipo muuguzi huyo kwani bado kuna utata kuhusu namna alivyotoweka nyumbani na mazingira ya tukio hilo yalivyokuwa.

“Kwa sasa hatuwezi kujua kwa kina kama ni utekaji au la, tukipata taarifa zote kwa kina tutaeleza. Hatuwezi kuthibitisha kama ni utekaji kwa sababu sisi hatujazungumza na watekaji zaidi ya kupata taarifa ya nesi huyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisema RPC Wambura.

Akizungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, muuguzi katika hospitali hiyo alisema Pili ni yatima na wengi hawakuwa wakiwafahamu ndugu zake wa karibu, jambo linaloweka utata zaidi kuhusu nani aliye nyuma ya utekaji huo na sababu za utekaji.

“Ana rafiki yake wa karibu hapa hospitali na huyo tu ndiyo tunamjua, sijawahi kusikia kuwa ana ugomvi na mtu au amefanya tukio la ajabu, kila mtu anashangazwa na hili tukio la kutekwa kwa Pili,”alisema.

No comments: