PROF. TIBAIJUKA ASAFIRI KWA BODABODA KM 13 NA KUWA MBUNGE WA KWANZA BAADA YA UHURU KUZURU KAAZI. - LEKULE

Breaking

28 Mar 2015

PROF. TIBAIJUKA ASAFIRI KWA BODABODA KM 13 NA KUWA MBUNGE WA KWANZA BAADA YA UHURU KUZURU KAAZI.


Mbunge wa Muleba Kusini, Prof Anna Tibaijuka alitembelea Kata ya Kimwani. kijiji cha Kaguramo kitongoji cha Kaazi Nyakishabo na kulakiwa na mamia ya wananchi waliopanda mlimani wakiwa na matawi ya miti huku wakiimba.

Kaazi pana kambi kubwa ya wavuvi. Mwenyekiti wa kitongoji cha Kaazi, Nyakishabo Ndugu Ojax Dorolyma Lyapa alionyesha furaha yake kwa kusoma risala ya kijiji kwa lugha ya kimombo huku akishangiliwa alipokuwa anaitafsiri. Mwenyekiti huyo alisema Prof. Tibaijuka ametengeneza historia kuwa Mbunge wa kwanza tangu uhuru kufika kwenye kijiji hicho kilicho mwambao wa ziwa.

Prof. Tibaijuka aliwasili Kyota majira ya saa 11 jioni akiwa amechelewa akitokea Bukoba ambapo alilazimika kuhudhuria kikao cha kamati ya siasa ya mkoa ya Chama Cha Mapinduzi ambamo yeye ni mjumbe.

Kwa ubovu wa barabara Prof. aliacha gari yake Kyota na kupanda pikipiki kilometa 13 hadi Kaguramo Mwisho ambapo alishuka na kutembea kilometa 2 kuteremka mlima mkali hadi Kaazi Nyakishabo.

Alishuhudia mamia ya watoto wa shule ya msingi wanaolazimika kutembea kilometa 7 kila siku kwenda shule ya msingi kaguramo.

Mwenyekiti wa kijiji aliomba Prof. Tibaijuka akubali kufadhili ujenzi wa shule ya msingi itakayojulikana kwa jina lake kijijini hapo. Bila kumungunya maneno mwenyekiti huyo wa CCM alimtaka Prof. kuendelea na Ubunge wa jimbo hilo kuleta maendeleo.

Prof. alianza hotuba yake kwa kuwataka watoto wasiokwenda shule kijitokeza. Mtoto Abdu alitoka mbele na kusema ameacha shule akiwa darasa la 3 kwa kukosa sare ya shule. Papo hapo Prof. Tibaijuka alitoa fedha za kumshonea sare. Prof. pia alichangia shilingi laki mbili na nusu kwenye mfuko wa kuwasaidia watoto wahitaji ili waendelee na masomo. Prof akaafiki kushirikiana na wanakijiji kujenga shule ya msingi baada ya kuambiwa kijiji cha Nyakishabo kina kaya 400. Prof alisema atawasiliana na Halmashauri kuhusu suala hilo.

Mwenyekiti wa kijiji aliorodhesha kero ya umeme, barabara na Prof akaafiki na kuahidi kuzifanyia kazi. Prof. alitoa michango mbalimbali kwa vikundi vya wanawake na vijana waliosoma risala zao, jumla ya milioni mbili na nusu.

Mkutano wa Kyota uliahirishwa baada ya kiza cha usiku kuingia, hata hivyo Prof. aliwasalimia wananchi waliomdubiri hadi usiku na kuahidi kurejea siku nyingine.

No comments: