Presha tupu, - LEKULE

Breaking

17 Mar 2015

Presha tupu,

Dar es Salaam. Ni presha kila kona ndivyo unavyoweza kusema kwa sasa jinsi Ligi Kuu Bara inavyoendelea katika mbio za ubingwa na wale wanaopigania kujinasua na janga la kushuka daraja msimu huu.

Mabingwa watetezi Azam, wamejitutumua na kupata ushindi mwemba wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Mshambuliaji Didier Kavumbagu ameendeleza makali yake kwa kufunga bao lake la 10 msimu huu na kuwahakikishia Azam pointi tatu muhimu. Ushindi huo unaifanya Azam kufikisha pointi 33, ikifutiwa na Yanga yenye pointi 31, Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 29.

Azam sasa inaongoza kwa pointi mbili ambazo si nyingi kwani Yanga nayo ina mechi dhidi ya Kagera Sugar kesho na ushindi utawarudisha kileleni.

Simba iliyo nafasi ya tatu imeziletea presha Yanga na Azam baada ya  kushinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Prisons, Yanga na Mtibwa na kujiweka katika mazingira ya kuwania ubingwa msimu huu ambao walikuwa hawatabiriki kutokana na matokeo yao mabovu katika mechi za awali.

Presha hiyo ilisababisha viongozi wa Azam kulilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwapangia mechi yao dhidi ya Ndanda kuchezwa jana badala ya Jumamosi kama walivyoomba.

“Unajua sasa hivi Ligi Kuu inaelekea ukingoni, inapendeza mechi zote zichezwe kwa wakati mmoja ili kukwepa kupanga matokeo. Sisi tunaelewa wenzetu Yanga wako kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho hivyo kutocheza mechi ya ligi wikiendi hii ni sawa, lakini kwa nini tusicheze siku moja na Simba Jumamosi,” alikaririwa akisema Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba.


Kwa muda mrefu, Yanga na Azam ndizo zilizokuwa zikikimbizana kileleni na zilikuwa tayari zimejiamini kuwa wao wawili ndiyo pekee wanaweza kutwaa ubingwa kutokana na matokeo ya kusuasua ya Simba, lakini sasa mambo yamebadilika.

“Nafurahia kiwango cha  timu yangu, naamini tutaendelea na mwendo huu, sasa hivi tunaweza kusema kuwa tunautaka ubingwa kwani tupo katika nafasi nzuri, ingawa Yanga na Azam wako juu yetu, lakini wanaweza kupoteza baadhi ya mechi kwani ndiyo maana ya ligi,” alisema Kocha wa Simba, Goran Kopunovic.

Hata hivyo, kikwazo kwa Simba kinaweza kuwa katika mechi chache walizobakiwa nazo tofauti na wapinzani wao Yanga na Azam, kwani Simba wamebakiwa na mechi nane, wakati Azam imebakiwa na mechi tisa na Yanga ina mechi 10.

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amekiri kuwa sasa ni muda wa kuwa waangalifu kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizo mbele yao kwani Simba wameongeza presha ya mbio za ubingwa.

“Muda mrefu nilisema hatupaswi kuidharau Simba, angalia sasa wako nyuma yetu na tunatofautiana kwa pointi chache   hivyo mbio za ubingwa zimekuwa za ushindani, cha kufanya ni kucheza kwa ungalifu kuhakikisha hatupotezi mchezo wowote kuanzia sasa,” alisema Pluijm.

Lakini si katika ubingwa tu ndio kwenye presha kwani hata kwenye timu zinazotaka kushuka daraja kuna presha pia na  Mkoa wa Mbeya unaweza ukaikosa Ligi Kuu msimu ujao kutokana na timu zake kuwa katika hatari ya kushuka daraja.

Mbeya City na Prisons zote zinashikilia mkia kwenye msimamo wa ligi na zinahitaji nguvu kubwa kujinasua katika janga la kushuka daraja, lakini pia timu kama Polisi Morogoro, Stand United, Mgambo Shooting na Ndanda nazo zote ziko katika hatari na yeyote atakayepiga mahesabu vizuri basi atabaki msimu ujao.

No comments: