NECTA YASOGEZA MUDA USAJILI WA WATAHINIWA - LEKULE

Breaking

18 Mar 2015

NECTA YASOGEZA MUDA USAJILI WA WATAHINIWA

BARAZA la Mitihani la Tanzania (Necta) limesogeza muda wa kujisajili kwa watahiniwa wa kujitegemea kwa ajili ya mtihani wa kidato cha nne.
Akizungumza na HabariLeo, Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi alisema hatua ya kusongeza mbele muda huo ni kutoa nafasi kwa watahiniwa kutafakari na kufikia uamuzi wa kufanya mtihani.
Alisema watahiniwa wa kujitegemea wamepewa muda wa kujisajili hadi Machi 31 mwaka huu, ambapo watasajiliwa bila kulipa faini.
Watahiniwa watakaojisajili katika kipindi cha kawaida watalipa ada ya Sh 50,000 kwa wanaojisajili mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na Sh 30,000 kwa wanaojisajili mtihani wa Maarifa (QT).
Awali, NECTA iliweka hadi Februari 28 mwaka huu kwa watahiniwa kujisajili kwa ajili ya mtihani wa Kidato cha Nne na Maarifa bila faini, kabla baraza hilo kuongeza mwezi mmoja wa watahiniwa wa kujitegemea.
Nchimbi alisema baada ya muda huo kupita, dirisha la usajili kwa ajili ya watahiniwa wa kujitegemea litakuwa wazi hadi Aprili 30, lakini watahaniwa watatakiwa kulipa na faini.
Aidha, Nchimbi aliwataka waombaji wote kuhakikisha kujisajili kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya Necta ya www.necta.go.tz na kuwa kabla ya kufanya hivyo wanatakiwa kwenda kwenye vituo wanavyokusudia kufanyia mtihani kuchukua namba rejea ambazo zinatolewa bila malipo.

No comments: