NEC Yaikana Kauli ya Mwenyekiti wake.......Yasisitiza Kuwa Kura ya Maoni Iko Palepale - LEKULE

Breaking

28 Mar 2015

NEC Yaikana Kauli ya Mwenyekiti wake.......Yasisitiza Kuwa Kura ya Maoni Iko Palepale

TUME ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) imesisitiza kwamba tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa ipo pale pale na hakuna mabadiliko yoyote kama inavyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey alisema kwa mara kadhaa baadhi ya vyombo vya habari vimenukuliwa vikiandika habari kuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Damian Lubuva amesema kura ya maoni kuhusu katiba haitafanyika Aprili 30 kama ilivyotangazwa awali.

Alisema hakuna mabadiliko yoyote na endapo kutakuwa na mabadiliko ya tarehe ya upigaji kura ya maoni kuhusu katiba inayopendekezwa taarifa rasmi itatolewa kwa umma.

“Kwa sasa kipaumbele kwa Tume ni kuhakikisha kuwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura linafanyika na kukamilika kwa ufanisi ili kuhakikisha kila mtanzania aliyetimiza miaka 18 anaandikishwa kwenye daftari,” alisema.

Aliongeza kuwa endapo daftari la kudumu la wapiga kura litakuwa halijakamilika hadi ifikapo Aprili 30 mwaka huu, tume itatoa taarifa rasmi ikiwa ni pamoja na kuelezea mwelekeo wa utaratibu huo katika Mikoa mingine.

No comments: