Musoma Vijijini ni moja kati ya wilaya sita zinazounda Mkoa wa Mara. Upande wa Kaskazini, inapakana na Tarime na Musoma Mjini, Upande wa Mashariki, kuna Wilaya ya Sengerema, Kusini kuna Wilaya ya Bunda na Magharibi inapakana na Ziwa Victoria.
Pia Musoma Vijijini ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Nimrod Mkono kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari hadi kwenye jimbo hilo ambalo kwa sasa makao makuu yake yapo Butiama na kuzungumza na wananchi mbalimbali walioeleza matatizo yanayowakabili.
MATATIZO YA WANANCHI
Matatizo yaliyoelezwa na wananchi kadhaa waliozungumza na gazeti hili, ni uduni wa elimu, ukosefu wa huduma bora za afya, kukosekana kwa maji safi na salama na ukosefu wa umeme jimboni humo kwa muda mrefu.
“Angalau Profesa Muhongo alipokuwa Wizara ya Nishati na Madini alikumbuka kwao kwa kutandaza nguzo za umeme sehemu mbalimbali, hata hivyo bado umeme haujawaka kwani kabla hajakamilisha kazi yake ndiyo sakata la Escrow likamuondoa madarakani, tunamuomba mbunge wetu atusaidie,” alisema Mwita Magafu, mkazi wa jimbo hilo.
Tatizo lingine kubwa linalowasumbua wananchi wa jimbo hilo, ni uduni wa elimu unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa, uhaba wa walimu, madawati na vifaa vya kujifunzia.
Elias Kajana Majinge ni Chifu wa Kabila la Wajita ambapo katika mahojiano na gazeti hili, alisema maendeleo ya elimu katika jimbo hilo yapo chini sana na yanazidi kuzorota kila kukicha huku kukiwa hakuna jitihada zozote za kuinua kiwango cha elimu jimboni humo.
“Zaidi ya wanafunzi 80 husoma katika darasa moja katika shule za msingi. Matokeo ya shule za sekondari ni mabaya mno, kwa mfano mwaka 2013, kati ya wanafunzi 1587 waliofanya mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne kutoka shule 17 za sekondari za kata, waliopata daraja la kwanza walikuwa saba tu,” alisema Majinge na kuongeza kuwa waliopata daraja la pili walikuwa 55, wakati daraja la tatu walikuwa 195, daraja la nne walikuwa 497, daraja sifuri walikuwa 628, hali inayotoa tafsiri halisi ya jinsi elimu ilivyo duni jimboni humo.
Majinge aliongeza kueleza kwamba wanafunzi wengi wa shule za msingi, huhitimu darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.
“Shule nyingi hazina madawati, hakuna madarasa hakuna walimu, hata kama wapo hawaingii madarasani,” alisema Majinge.Wananchi wa Musoma Vijijini walieleza pia kuwa kero nyingine inayowasumbua ni ukosefu wa huduma za afya, ambapo kuna kituo kimoja tu cha afya jimbo zima kiitwacho Murangi pamoja na zahanati kadhaa ambazo hata hivyo hazikidhi mahitaji ya wananchi wote wa jimbo hilo, huku kukiwa hakuna hospitali kubwa hata moja.
“Kama una mgonjwa wako amezidiwa, inabidi mumbebe kwenye machela kwenda Musoma Mjini au Bunda, huko ndiyo kuna hospitali, vinginevyo atakufa huku mkishuhudia, Kituo cha Afya cha Murangi hakina dawa wala wauguzi wa kutosha, hizo zahanati ndiyo usiseme. Tunaomba serikali itusaidie jamani,” alisema Marwa Mturo mkazi wa jimbo hilo.
“Pia hili jimbo lina migogoro mingi ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima na kuna wakati kuliwahi kutokea mapigano yaliyosababisha vifo. Tunamuomba Mkono atimize ahadi zake alizotuahidi wakati akiomba kura,” alisema Issa Rajab, mkazi wa Saragana.
Kero nyingine ambayo Uwazi iliibaini, ni ukosefu wa maji safi na salama licha ya kwamba jimbo hilo linapakana na Ziwa Victoria pamoja na Mto Mara. Wananchi wengi hunywa maji ya ziwani pamoja na ya kwenye mito, ambayo pia hutumika kunyweshea mifugo na kilimo jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya zao.
Baada ya kusikiliza kero za wananchi, Uwazi lilimtafuta Mheshimiwa Mkono ambaye mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, namba yake ya simu haikuwa ikipatikana hewani. Hata hivyo, jitihada za kumtafuta bado zinaendelea ili atoe ufafanuzi wa kero zilizoainishwa na wananchi wa jimbo lake.
No comments:
Post a Comment