MSIMU WA KTMA 2015 WAZINDULIWA RASMI - LEKULE

Breaking

23 Mar 2015

MSIMU WA KTMA 2015 WAZINDULIWA RASMI


Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza, akizungumzia jinsi baraza hilo lilivyoboresha baadhi ya vitu kwenye tuzo hizo ambazo zinatarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi huu.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikoli, akielezea namna ya mchakato wa tuzo za Kilimanjaro Music Awards kwa mwaka huu jinsi zitakavyofanyika.

Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini baadhi ya mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea kwenye kikao cha uzinduzi huo.

MUDA wa utoaji tuzo kwa wasanii wa Tanzania wanaofanya vizuri umewadia na tayari mchakato wa awali wa mchanganuo wa tuzo hizo zinazojulikana kama Kili Tanzania Music Awards 2015 (KTMA) umetangazwa rasmi leo.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli, ambao ndiyo wadhamamini wakuu wa tuzo hizo kupitia usimamizi wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), aliweka wazi kuhusiana na mchakato mzima wa mwaka huu utakavyokuwa kwenye hafla fupi iliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa LAPF uliopo Kijitonyama, Dar es Salaam.

Kikuli alifafanua kuwa kuna vitu vingi vimeongezeka katika msimu, huu lengo likiwa ni kuboresha utoaji na zoezi zima la tuzo hizo. Mojawapo ni kuwapa fursa Watanzania kupendekeza wasanii watakaowania tuzo hizo kwa kuwapigia kura waingie kwenye kinyang’anyiro kwa njia tatu kuu.

“Tumekuwa na juhudi za makusudi za kutenga fungu kubwa na kuongeza ushiriki wa wataalam mbalimbali kwenye fani husika ili kuziendeleza, kuzikuza na kuziongezea thamani tuzo hizi mwaka hadi mwaka sambamba na umaarufu kuongezeka kwenye medani za kimataifa.

“Wananchi watapata fursa ya kupiga kura kupendekeza wasanii katika vipengele mbalimbali kwa kutumia njia tatu; kwa mfumo wa Website ya www.ktma.co.tz, mfumo wa mtandao wa WhatsApp na kwa njia ya SMS pia,” alisema Kikuli.

Aidha katika mfumo mpya wa WhatsApp mpiga kura ataweza kutumia namba ya 0686 528 813 na SMS pia kutumia namba 15415 kwa kutuma ujumbe wa neno KTMA au KILI na kisha kufuata maelekezo kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo litaloanza rasmi Machi 30 mpaka Aprili 19, mwaka huu litakapositishwa.

Baada ya upigaji wa kura hizo kutakuwa pia na michakato mingine itakayofuata katika kuwatafuta washindi mpaka mwisho wa utoaji wa tuzo hizo kama kuchuja wapendekezwa kabla ya kuwarudisha tena kwa wananchi na kupigiwa kura za ushindi kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.

No comments: