Mwandishi wa Blog hii akirekodi matukio katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine kati ya Mbeya City na Ruvu Shooting timu hizo zilizotoka sare ya 1-1.
Golikipa wa timu ya Ruvu Shooting akiwa ametoka golini kuufuata mpira katikati ya uwanja huku mchezaji Hamis Kasanga wa Shooting na Hamad Mohamed wa Mbeya City wakiwania mpira huo.
Kikosi cha Ruvu Shooting kilichochuana na Mbeya City jana
Kikosi cha Mbeya City kilichochuana na Ruvu Shooting
Manahodha wa timu za Ruvu na Mbeya City wakikumbatiana kabla ya kuanza kwa mechi kati ya timu zao ndani ya uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine jana
Bao la winga wa kushoto Themi Felix aliyevalia jezi nambari 7 mgongoni lililofungwa kunako dakika ya 70 ya mchezo wa ligi kuu ya Vodacom ndani ya uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ndilo lililoepusha kizaazaa kingine kuibuka kwa timu ya Mbeya City.
Felix ambaye anaweza kuwa ndiye mkombozi wa Mbeya City kuadhiriwa nyumbani kwa mara ya pili mfululizo baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha 3-1 kutoka kwa wakongwe wa ligi hiyo nchini Dar Young African wiki iliyopita.
Nderemo na vifijo vya mashabiki wa timu hiyo iliyojizoelea mashabiki lukuki ndani na nje ya mkoa wa Mbeya zilikuwa zimefifia baada ya kutandikwa bao la kwanza na timu ya Ruvu Shooting yenye sifa ya viongozi wake kuwa na majigambo ya kuwapa moyo wapenzi wake hata kama inakabiliana na mechi ngumu na kubwa kiasi gani.
Kufifia kwa nderemo hizo kulitokana na timu ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani kujipatia goli dakika 11 tu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji Yahya Tumbo aliyefunga bao kwa tiktaka baada ya kupata krosi maridadi kutoka kwa mchezaji mrefu kuliko wote katika mchezo huo Botram Mwombeki.
Bao hilo lilivunja ukimya kwa mashabiki wachache wa Ruvu Shooting ambao asilimia kubwa walikuwa ni askari kutoka kikosi cha JKT Itende na kuanza kushangilia huku wakiranda huku na kule kuwapa nguvu wachezaji wa Shooting.
Bao hilo ambalo lilidumu kwa dakika 51 liliwakatisha tamaa mashabiki wa Mbeya City na hata kuonekana mithili ya walionyeshewa na mvua huku wachezaji wa timu hiyo pamoja na kocha mkuu Juma Mwambusi kiroho kikiwadunda.
Aliyeonekana kuwa na wakati mgumu katika mchezo huo ni Kocha Mwambusi ambaye bila ya shaka alikuwa akihofia kibarua chake kuota nyasi kutokana na kuonekana timu hiyo ikiendelea kufanya vibaya bila kutafutiwa ufumbuzi kwa tatizo hilo.
Aidha goli hilo pia lilionekana kama ni faraja kwa kipa aliyesimamishwa wa timu ya Mbeya City David Burhani kutokana na kile kilichoelezwa alisababisha timu yake kufungwa bao na Yanga alipokuwa akichezea mpira golini na mchezaji wa Yanga Mrisho Ngasa kuukwamisha mpira kimiani katika mchezo baina ya timu hiyo na Yanga wiki iliyopita.
Kipindi cha pili cha mchezo kilianza kwa kila timu kufanya mashambulizi kwenye lango la mwenzie lakini ilikuwa ni timu ya Mbeya City iliyofanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni kwa Ruvu na kuonekana kama vile wameanza kuonana katika mchezo.
Matunda ya kuelewana katika kipindi cha pili yaliyochangiwa na mabadiliko ya wachezaji ambapo mchezaji Deus Kaseke alitoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji machachari mwenye tabia ya kurusha mpira kama kona Hamad Kibopile.
Kibopile alionesha uhai mkubwa katika safu ya ushambuliaji na wachezaji wa Mbeya City kuanza kuonana vyema ambapo katika dakika ya 70 mchezaji Themi Felix aliwainua mashabiki uwanjani kwa kufunga bao safi baada ya kuunganishiwa pasi kutoka kwa Kibopile na hivyo kusawazisha bao 1-1.
Baada ya bao hilo wachezaji wa Mbeya City walionesha uhai katika mchezo huku wachezaji wa Ruvu wakionekana kutoelewana ilhali golikipa wa timu hiyo Abdallah Abdallah akidaka mpira na kuutema mara kadhaa.
Mbeya City ambao walimpanga golikipa Hanington Kalyesebula alionekana kukukumbana na vikwazo vya kuzoea goli kutokana na muda mrefu kuwa benchi huku golikipa pekee aliyekuwa akipangwa mara kwa mara akiwa ni Burhani ambaye kwa sasa amesimamishwa.
Kila timu ilifanya mabadiliko kwenye mchezo huo kwa timu ya Mbeya City mbali na kuingia Kibopile badala ya Kaseke,Peter Mapunda aliingia badala ya Hamad Mohamed ilhali kwa upande wa Shooting Mwombeki alitoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Mwita John.
Kama ilivyo ada baada ya kumalizika kwa mchezo huo hakukosekana kwa maneno ya lawamna za mchezo huo ambapo Kocha Juma Mwambusi aliulaumu uongozi wa TFF kuipangia timu yake mwamuzi Athumani Lazi(Moro) ambaye ndiye aliyechezesha mechi kati ya Mbeya City na Yanga wiki iliyopita na ndiye huyo huyo aliyechezesha mechi kati ya timu hiyo na Coastal Unioni mjini Tanga.
''TFF iangalie hili, refa mmoja tunapangiwa kwa mechi zote ambazo tunafanya vibaya kama vile wana ajenda yao kutaka timu yetu ifanye vibaya katika ligi hii,''alisema Mwambusi.
No comments:
Post a Comment