Dodoma. Vurugu, matusi ya nguoni, kejeli, kelele na zomeazomea vilitawala jana katika semina ya wabunge kuhusu Muswada wa Sheria ya Mahakama ya Kadhi, baadhi wakitaka uwasilishwe bungeni kama ilivyopangwa na wengine wakitaka uondolewe, hali iliyosababisha baadhi yao kutaka kupigana.
Semina hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na kufanyika katika ukumbi wa Msekwa, ilianza saa 5.04 asubuhi hadi saa 10.20 jioni, huku wabunge wakiishushia lawama Serikali, hususan Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kutaka kuwasilisha muswada huo bungeni bila kuwashirikisha, kwa kina, Waislamu na Wakristo.
Katika mvutano huo nusura Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali ashikane mashati na Mbunge Konde (CUF) Khatib Said Haji na Mbunge wa Chwaka (CCM) Yahya Kassim Issa baada ya kupishana kauli.
Semina hiyo iliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, William Ngeleja ilihudhuriwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri Mkuu Pinda, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju huku Jaji Dk Robert Makaramba wa Mahakama Kuu akipewa jukumu la kutoa mada kuhusu Mahakama ya Kadhi.
Hali ya kutoelewana ilianza kuonekana hata kabla ya kuanza kwa semina hiyo kutokana na wabunge wengi kupanga kukwamisha muswada huo kujadiliwa bungeni kwa madai kuwa utaleta udini na kuligawa Taifa.
Wabunge waliotoa maneno makali katika semina hiyo ni Mbunge wa Fuoni (CCM), Said Mussa Zubeir na Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage.
Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jaffo alipokuwa akichangia kuwataka wabunge Waislamu kukutana baada ya semina hiyo.
“Serikali isifanye masihara juu ya muswada huu. Wanachotakiwa kufanya ni kukubali ujadiliwe bungeni na huko bungeni ndiyo tufanye marekebisho,” alisema Jaffo.
Kauli hiyo ilipingwa na Machali ambaye alimwambia anazungumza kitu ambacho hakijui, kitendo ambacho kilisababisha Yahaya Kassim Issa na Khatibu Saidi Haji kusimama kwenye viti vyao na kwenda ‘kumtia adabu’, kabla ya kuzuiwa na wenzao waliokuwa karibu nao.
Vurugu na kelele viliendelea kwa takribani dakika 20 huku baadhi ya wabunge wakitoka nje ya ukumbi huo licha ya kutakiwa kutofanya hivyo na Spika Makinda. Kutokana na hali hiyo, Polisi walilazimika kuingia katika ukumbi huo kwa lengo la kutuliza vurugu.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu alisema Waislamu wanapaswa kulia na Pinda kuhusiana na Mahakama ya Kadhi.
“Waislamu nawaambia kama mtu wa kulia naye ni Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye ndiyo chanzo cha kutopatikana,” alisema.
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa aliishauri Serikali kurudisha muswada huo na kwenda kuuangalia kwa mapana yake badala ya kuuwasilisha bungeni.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alitaka Waislamu waachwe wenyewe katika masuala yanayohusu imani yao. Alimshukia Pinda akisema ‘amechemka’ kwa kuwaahidi Waislamu kuwa atapeleka muswada huo bungeni, akihusisha suala hilo na mbio za Pinda kuutaka urais.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy alisema hakubaliani na suala la kuitambua Mahakama ya Kadhi kisheria akisema hiyo si miongoni mwa Nguzo Kuu za Uislamu.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alikosoa kauli ya Serikali kuwa haitaihudumia Mahakama hiyo, akieleza kuwa upo waraka wa Serikali (huku akiionyesha) ambao pamoja na mambo mengine unaonyesha kwamba itasaidia uanzishwaji wake kwenye hatua za awali.
Akifunga semina hiyo, Pinda alisema baada ya kuwasikiliza wabunge hao ametambua kuwa ndani ya Waislamu wenyewe hakuna maelewano juu ya uanzishwaji wa Mahakama hiyo. Alisema baada ya kuona hali hiyo, Serikali italitizama upya suala hilo na kuona inalitatua vipi.
“Pia nimebaini baadhi ya watu wanafikiri kwamba sheria iliyotungwa na Serikali ni kilemba cha ukoka kwa Waislamu. Wengine wanadhani baadhi ya Waislamu hatujawafikisha pale wanapotaka, lakini hiki ni matokeo ya mjadala ulioibuka ndani ya Bunge la Katiba,” alisema. Alisema wasiwasi mwingine ni ule wa kuona kwamba inawezekana kuna kilichojificha nyuma ya muswada huo na kwamba baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo mambo mengine yaingizwe kimyakimya.
“Jambo hili sisi serikalini tutakaa tuone cha kufanya. Nisingependa twende mbele ya mama Makinda na tuanze kunyoosheana vidole. Tutashauriana na Spika na baadaye Rais (Jakaya) Kikwete ili tuone ni nini cha kufanya ili kuweza kufikia muafaka vizuri,” alisema.
No comments:
Post a Comment