Dar es Salaam. Jukwaa la Wakristo Tanzania limewataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya “hapana”.
Taarifa iliyotolewa na Jukwaa hilo jana na kusainiwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet, imetaja sababu mbili za uamuzi wake kuwa ni muswada wa Mahakama ya Kadhi kukiuka misingi ya Taifa kuwa na Serikali isiyo na dini, na Kura ya Maoni kusababisha mgawanyiko.
“Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana kwa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa hapo juu,” linasema tamko hilo la kurasa nne.
Taarifa hiyo imekuja siku moja tu baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza kuwa muswada wa uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi uliokuwa umeondolewa kwenye mkutano uliopita wa Bunge kwa ajili ya mashauriano zaidi, utawasilishwa katika vikao vya chombo hicho vinavyoanza Jumanne ijayo baada ya kufikiwa kwa maridhiano baina ya viongozi mbalimbali wa dini.
Pia tamko hilo limekuja siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuiagiza Hazina itoe fedha kwa Tume ya Uchaguzi (Nec) kwa kadri inavyohitaji ili kuiwezesha kukamilisha mchakato wa Kura ya Maoni.
Viongozi wa Jukwaa la Wakristo walikutana Machi 10, mwaka huu kujadili kwa kina kuhusu hali ya usalama wa nchi ilivyo sasa na mustakabali wake, Katiba inayopendekezwa na uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi.
Katiba inayopendekezwa
Taarifa hiyo ya maneno 712 inasema: “Katiba Inayopendekezwa imeleta mgawanyiko mkubwa katika Taifa kwani imepatikana kwa njia zisizo za kiadilifu na mchakato wake umeendeshwa kwa hila na ubabe.
“Pia haijajibu matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye masuala mbalimbali kama muundo wa Serikali, miiko na maadili ya viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya rais na uwiano wa mihimili ya dola.
“Ikumbukwe Katiba Inayopendekezwa ilipitishwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwa ahadi ya Serikali kuipa dini ya Kiislam Mahakama ya Kadhi. Inashangaza kuwa hata Serikali inatoa rushwa ili kufikia malengo yake. Kwa hali kama hii, Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Mahakama ya Kadhi
Kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, taarifa hiyo inasema, “Suala la uanzishwaji wa Mahakama hii nchini kama tulivyotoa maoni yetu kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria (Januari 16, 2015); barua yetu kwa Waziri Mkuu na matamko mbalimbali yaliyokwisha kutolewa kuhusu jambo hili; Mahakama ya Kadhi inakiuka misingi ya Taifa hili kuwa na Serikali isiyokuwa na dini wala mfumo wa sheria unaobagua raia wake kwa misingi ya dini.”
Inaeleza kuwa mjadala unaoendelea unavunja Katiba ya Jamhuri Ibara ya 19 kwa kuendelea kujadili suala hilo katika Ilani za vyama vya Siasa, majukwaa ya kisiasa na bungeni na kusisitiza kuwa suala hilo limeligawa Taifa, Serikali, Bunge, Mahakama na wananchi.
“Mahakama ya Kadhi imekuwa ikiendelea kutumiwa na wanasiasa kama mtaji wao wa kujipatia madaraka kwa gharama za kuleta chuki za kidini.
“Kwa dhamiri safi, Jukwaa linatamka wazi kuwa mjadala unaoendelea kati ya Serikali na vikundi vya kidini kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kikatiba na kisheria ufungwe na badala yake ziachiwe taasisi husika za kidini kuamua juu ya masuala hayo bila kuihusisha Serikali wala waumini wa dini nyingine,” inasema taarifa hiyo.
Hali ya usalama
Kuhusu hali ya usalama nchini Jukwaa hilo limeeleza kusikitishwa na viashiria pevu vya ugaidi vilivyoanza kujitokeza nchini kwa takribani miaka mitano iliyopita na kwamba kumekuwa na vitendo vinavyoashiria kuchipuka kwa ugaidi nchini.
Maaskofu hao wameyataja matukio kama vile uvamizi wa vituo vya polisi, kuporwa silaha na mauaji ya polisi, mafunzo ya kareti katika nyumba za ibada, mafunzo ya itikadi kali za kidini kwa watoto, tukio la Amboni Tanga, mauaji ya viongozi wa dini, uchomaji wa nyumba za Ibada na kumwagiwa tindikali kwa viongozi wa dini.
“Jukwaa linasikitishwa na mwendelezo wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (maalbino) na ukatili unaosababisha ulemavu wa kudumu wa maalbino katika nchi yetu. Hali hii inatishia utulivu, amani na umoja wa kitaifa tuliokuwa nao kama Taifa la mfano barani Afrika,” inaeleza taarifa hiyo.
Jukwaa hilo limewataka wananchi kuacha tabia ya kuua albino na kusisitiza kuwa kukosekana kwa uwajibikaji wa viongozi wa Serikali na kuongezeka kwa wigo wa kipato kati ya walionacho na wasionacho kunachangia ongezeko la vitendo hivyo viovu.
“Mbona tembo na ng’ombe wakiuawa operesheni maalumu zinafanyika na viongozi wanawajibika, kwa nini maalbino wakiuawa viongozi hawawajibiki,” inahoji sehemu ya taarifa hiyo.
“Kwa kuwa chama tawala na Serikali wameshindwa kusimamia misingi iliyolea taifa kama serikali isiyo ya kidini na taifa lenye amani; umoja na utulivu; Jukwaa linawaelekeza waumini wote na wenye mapenzi mema wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao kufanya maamuzi yanayolitanguliza Taifa badala ya kutanguliza mazoea, mapokeo, itikadi na ushabiki wa chama fulani cha Siasa.”
No comments:
Post a Comment