KUELEKEA UCHAGUZI MKUU: Wanaokata majina ya wagombea CCM marufuku - LEKULE

Breaking

7 Mar 2015

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU: Wanaokata majina ya wagombea CCM marufuku



Mpwapwa. Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amepiga marufuku viongozi wa chama hicho katika ngazi zinazofanya uteuzi wa wagombea kukata majina ya watu walioomba nafasi mbalimbali ili kukinusuru kisipoteze nafasi nyingi.

Kinana alisema tabia za watu kujiona na kufanya uongozi wa kifalme ndani ya CCM inapaswa kukomeshwa kwa kuwa chama hicho ni cha watu na kila mtu ana haki ya kuwa kiongozi ilimradi awe na sifa.

Kinana alitoa kauli hiyo juzi wakati akipokea taarifa ya CCM Mkoa wa Dodoma katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani hapa. Ziara hiyo ilianza juzi na imepangwa kumalizika Machi 13.

Kuchukua hatua

Katibu Mkuu alisema kuwa tabia kama hizo hazivumiliki ndani ya chama hicho kwa sasa na ndiyo maana hata uongozi wa CCM taifa umeacha kuwafumbia macho baadhi ya watu wanaoonekana kukaidi na kwenda kinyume na maadili ya chama.

Kiongozi huyo aliagiza CCM kufanya tathimini na uchunguzi wa kina na ikibainika kuna viongozi waliohusika na kukata majina ya baadhi ya wagombea wachukuliwe hatua za kinidhamu.

“Hata sisi ngazi ya juu si mlisikia kuwa tuliwawajibisha na kuwaonya watu walioanza kwenda kinyume na maadili ya chama, je ninyi mnashindwa nini kushughulika na watu ambao mnaamini walifanya kinyume na kusababisha chama kupoteza nafasi?

“Mnajua kikao cha Kamati Kuu kilichokutana kule Zanzibar kilikaa na kuwajadili watu ambao tunaona wanakwenda kinyume. Hivi kama sisi tumeanza nyinyi mnangoja nini sasa?” alihoji Kinana.

Aliwaagiza viongozi wote kutenda haki katika uchaguzi ujao ili kuondoa manung’uniko mengi kiasi cha kukipa mzigo chama.

Watendaji wa Serikali

Kuhusu suala la watendaji serikalini, Kinana alisema Watanzania wamechoshwa na maneno ya Serikali, wanachohitaji ni utekelezaji wa kazi kwa vitendo.

“Watu wamesubiri kwa muda mrefu sasa wamechoka, hawataki tena maneno kinachotakiwa ni utekelezaji na kuona vitu vikifanyika,” alisisitiza.

Kauli ya Kimbisa

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Adam Kimbisa alisema kauli ya Kinana ni sawa na agizo, amejipanga kurudisha majina ya watakaoshinda.

Kinana alisema hakuna mtu atakayekatwa jina iwapo atakuwa ameongoza katika kura za maoni kwa kuwa hata yeye anatambua kuwa jambo hilo kwa sehemu kubwa limewapunguzia kura na kushindwa katika baadhi ya maeneo wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema kazi waliyonayo mwaka huu ni kuhakikisha CCM inashinda katika kata zote na majimbo tisa ya ubunge.

Madeni ya maji

Katika mkutano wa hadhara juzi wilayani Mpwapwa, wananchi walitoa malalamiko kuhusu huduma mbovu ya maji wakiitaja kuwa ndiyo kero yao namba moja.

Kutokana na malalamiko hayo, Kinana alimwita Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji ya Mpwapwa, Shedrack Matemba na kumtaka atoe maelezo. Alisema tangu Septemba mwaka jana, taasisi za Serikali zinadaiwa Sh174.3 milioni wakati deni la wananchi wa kawaida ni Sh1 milioni.

Mkurugenzi huyo alisema juhudi za kudai madeni hayo zimekwama kutokana na majibu yanayotolewa na taasisi husika.

“Jamani kuna wengine wanatia aibu kweli, hebu tazama hapa miongoni mwa wanaodaiwa ni TRA, NMB, Tanesco, Idara ya Elimu na CRDB pamoja na wengine nikiwataja ni aibu, hivi tunakwenda wapi,” alihoji Kinana.

Baada ya maelezo hayo, Kinana alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa kufanya kila mbinu kuhakikisha wadeni hao wanalipa fedha hizo ili mamlaka hiyo iendelee kutoa huduma

No comments: