Kiswahili dhidi ya Kiingereza au Kiswahili pamoja na Kiingereza? - LEKULE

Breaking

13 Mar 2015

Kiswahili dhidi ya Kiingereza au Kiswahili pamoja na Kiingereza?


Suala la matumizi ya lugha Tanzania limeleta ushindani mzito kati ya Kiswahili na Kiingereza.

Hoja ya watetezi wa Kiingereza inajumuisha pia madai kuwa kuendelea kutumia Kiswahili, ni kuwafanya Watanzania washindwe kushindana kiuchumi katika dunia ya leo.

Dunia ya leo ni dunia ya utandawazi ambapo mipaka baina ya mataifa inapuuzwa na watu wanaweza kuwekeza, kuajiriwa na kufanya biashara karibu popote duniani.

Kwa sababu hiyo Kiingereza kinawafungulia milango katika dunia ya utandawazi. Lakini tusije kusahau watu wengi kutoka nchi nyingi wanakitumia Kiingereza kama lugha ya kibiashara na mawasiliano na watu ambao hawajui lugha yao ya kitaifa. Watu hawa wakiwa katika nchi zao wanatumia lugha zao za taifa.

Mifano ni pamoja na Wajerumani, Wajapani, Wafaransa, Waitalia, Wachina, Warusi na wengineo.

Ninavyoona mimi ni kwamba uzito wa hoja ya wale wanaopendekeza Kiingereza iwe lugha ya kufundishia Tanzania, unatokana na hoja ya umuhimu wa lugha hiyo katika uchumi wa viwanda.

Msingi wa lugha ni fikra zinazoelezwa katika maneno ambayo yanadhihirisha mkakati wa mpango fulani. Endapo mchakato wa mpango hauridhiki katika kasi ya mwenendo wake, lugha inaweza kurekebisha na kuongoza kutokana na msingi wa lugha husika kuwa desturi za wote wanaohusika ambao wamekipa kipaumbele matumizi yake.

Changamoto iliyopo katika maendeleo ya matumizi ya Kiswahili ni kuendeleza fikra za Watanzania. Fikra zitakazoeleza vitendo endelevu ambavyo vitasukuma mbele uchumi wa Tanzania na kuboresha maisha ya Watanzania.

Tukumbuke moja ya maneno maridhawa ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeahi kuandika kitabu akakipa jina la “We Must Run While They Walk. Alimaanisha Tukimbie wakati wenzetu wakitembea.

Hoja yangu ni lugha ipi inawasukuma Watanzania kukimbia kati ya Kiswahili na Kiingereza? Jibu la kimsingi ni zote hizo mbili. Uchaguzi uliopo ni wa njia. Kila lugha husika ina njia inayoweza kutumika kufikia malengo ya matumizi yake kwa ufanisi. Lakini pia tujiulize kama njia hiyo inajenga maadili ya kudumu nchini Tanzania?

Nashauri iwe njia ya kufuata au njia ya kuongoza ambayo itajenga utaifa Tanzania. Kiswahili kikiwa lugha ya chimbuko la Utanzania kinaweza kuongoza.

Kiingereza ni lugha ya uvamizi wa ardhi ya Afrika, haina budi iwe ya lugha ya pili. Wasichoelewa watu wengi ni kuwa Kiingereza kinaweza kusaidia katika dunia ya utandawazi, lakini hakina uwezo wa kujenga Utanzania.

Msingi wa uthibitisho wa hoja yangu nautolea mfano nchini Uingereza. Kwa nini Mfalme Henry VIII alikifanya Kiingereza kuwa lugha rasmi ya Uingereza akiipinga lugha ya Kilatini iliyotumiwa na jamaa wa mfalme, watu wa tabaka ya juu, matajiri, wasomi na wataalamu?

Kiingereza kilikuwa lugha ya sokoni, lugha ya kina yakhe, Ilikuwa lugha ya kuongea na watumishi na wahudumu nyumbani.

Kiswahili hata katika taaluma kinawezekana na kwa mfano, hakuna haja ya kutafsiri istilahi za sayansi, tiba au hesabu. Tukumbuke hata Kiingereza bado kinatumia istilahi za Kilatini katika fani hizi.

Wataalamu Waingereza waliendelea kutumia Kilatini katika fani hizo hata baada ya mapinduzi ya kilugha Uingereza.

Aidha, sioni haja kwa mfano tutohoe neno pressure na kuita presha, ilhali tunaweza kusema shinikizo

Pete Mhunzi ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika na mpenzi wa Lugha ya Kiswahili 

No comments: