Kesi ya Mtikila Kupinga Mahakama ya Kadhi yapangiwa Jaji. - LEKULE

Breaking

27 Mar 2015

Kesi ya Mtikila Kupinga Mahakama ya Kadhi yapangiwa Jaji.

Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepanga Machi 30, mwaka huu kusikiliza kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila, akipinga kitendo cha Serikali kupeleka Muswada bungeni wa kutunga sheria ya kuanzishwa Mahakama ya Kadhi, kwamba uko kinyume na Katiba ya nchi.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Richard Mziray.

Katika kesi hiyo, Mtikila ameiomba mahakama itoe amri kwamba wale walio kwenye mamlaka ya Serikali  akiwaemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Mary Nagu; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,  Stephen Wasira na wenzao watoe sababu kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka mitano endapo watashindwa kujieleza.

Pia, Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14 ya mwaka huu, ameomba mahakama itoe amri ya vigogo hao kufungwa kifungo hicho kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.

Pia, Mtikila anaiomba, Mahakama itoa amri kwamba Mahakama ya Kadhi na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC) itangaze ni haramu kwenye ardhi ya Tanzania.

Kadhalika, anadai kuwa suala la serikali kuandaa muswada wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo cha Bunge kukubali ni sawa na uhaini.

Anadai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo walivyoapa viongozi hao wakati wa kushika madaraka ya umma na ni kinyume cha ibara ya 19 ya katiba ya nchi inayoeleza kwamba masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kwamba uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya nchi

No comments: