Dar es Salaam. Huwezi kumzungumzia John Damiano Komba kwa kirefu bila ya kutaja kikundi cha uhamasishaji cha CCM cha Tanzania One Theatre (TOT), msimamo wake na tuhuma ambazo zimekuwa zikimuandama katika siku za karibuni, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Komba (60), mwanajeshi mstaafu na mwimbaji kinara wa kikundi cha Tanzania One Theatre, alifariki jana kwa ugonjwa wa kisukari akiwa hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kifo chake zitakuwa zimegusa wote wanaomfahamu kwa mambo hayo, na kwa kuwa kipindi hiki nchi inajiandaa kupata rais mpya, lakini kazi yake kubwa ya kuipigia debe CCM si rahisi kutambuliwa.
Mwanajeshi huyo aliyestaafu akiwa na cheo cha kepteni alikuwa ni mtu ambaye hakusita kueleza kile alichokiamini, jasiri asiyekubali kushindwa, mcheshi wakati fulani na mtu mwenye msimamo.
Komba alianza kupata umaarufu akiwa na kikundi cha burudani cha JWTZ wakati huo akiwa hajastaafu jeshi.
Alizunguka na kikundi hicho kila sehemu ya nchi akiwa mwimbaji kiongozi wa kwaya ya kikundi hicho, ambacho pia kilikuwa na sanaa za sarakasi, maigizo na taarab.
Lakini wakati nchi iliporejea kwenye mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, kikundi hicho kiliondoka jeshini na kuingia CCM na ndipo kilipobatizwa jina la Tanzania One Theatre (TOT).
Jina la kikundi hicho ndilo lililoifanya CCM ijinadi kwa jina la Nambari One kwenye kampeni za mwaka 1995 wakati Benjamin Mkapa aliposimama kwa tiketi ya CCM kuwania urais.
Aliendeleza kikundi hicho na kupata umaarufu, hasa kiliposhindana na Muungano Theatre iliyokuwa maarufu kwa taarab. Katika kipindi hicho, ndipo alipoanzisha staili ya Achimenengule (tucheze) kwenye bendi ya muziki wa dansi ya TOT, ambayo ilikuwa kiasi cha kupambana na bendi nyingine maarufu kama African Stars na Mchinga Sound.
Lakini umaarufu wake ulikuwa kwenye siasa ambako Kepteni Komba alitunga nyimbo nyingi za kuipigia debe CCM ambazo ziliimbwa karibu nchi nzima, hata sehemu ambazo TOT haikuwapo.
Katika miaka ya karibuni, Komba amejikuta kwenye matatizo kutokana na misimamo yake mikali na pia habari za mwandani wake kuandikwa sana na mitandao ya kijamii.
Ni hivi karibuni tu alikuwa akihojiwa na moja ya redio za FM akieleza mkakati aliouanza kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya kutoa wimbo wa kuhamasisha wananchi kupigia kura wagombea wa CCM.
Lakini katikati ya mahojiano hayo akatumbukiza msimamo wake kuhusu mgombea urais akimuelezea kuwa “ndio jembe la CCM” kwenye Uchaguzi Mkuu ujao.
Hakutaja jina lake, lakini katika mikutano mbalimbali amekuwa akieleza kuwa Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani, ndiye chaguo sahihi la mgombea urais kwa tiketi ya CCM na amekuwa akibainisha kuwa atasimamia hilo hadi mwisho, lakini akibainisha kuwa iwapo hatapita, atakuwa tayari kumpigia debe mteule mwingine.
Kama kawaida yake, alimaliza kwa kuisifia CCM kuwa ndicho chama pekee kinachoweza kutoa rais anayeifaa Tanzania.
Msimamo wake hauonekani katika mgombea urais tu. Wakati wa vikao vya Bunge la Katiba, Komba aliungana na wajumbe wengine kutoka CCM waliomshambulia Jaji Joseph Warioba kwa maneno makali kupinga mapendekezo ya muundo wa Serikali ya Muungano yaliyokuwamo kwenye Rasimu ya Katiba.
“Mimi nasema ukweli kabisa, huyu mzee ana nini, ana kitu gani na sisi, mbona anatuingilia sana,” alisema.
Mbunge huyo, ambaye kitaaluma ni mwalimu, alienda mbali zaidi aliposema iwapo muundo wa serikali tatu utapitishwa, “ataingia msituni”, kauli ambayo ilisababisha wabunge wengine kumpinga.
Pia, alishambulia wajumbe wengine wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Salim Ahmed Salim na Joseph Butiku kutokana na makada hao wa CCM kuwa na msimamo tofauti na yeye katika suala la Muungano.
Hakupata bahati ya kuandikwa vizuri kwenye mitandao ya kijamii ambako habari kuhusu faragha yake ziliandikwa sana, hasa uhusiano wake na wasanii wa kike na wakati mwingine hata picha zake kusambazwa.
Tukio linaloonekana kuwa kubwa ni lile la kunadiwa kwa mali zake kutakiwa kupigwa mnada kwa kile kilichoelezwa kuwa ni deni la takriban Sh900 milioni alilokuwa akidaiwa na benki ya CRDB.
Komba, ambaye aliingia kwenye ujasiriamali na kumiliki shule na biashara mbalimbali, alionekana kutetereka katika miaka ya karibuni. Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati kampuni ya Mpoki and Associates ilipotoa tangazo gazetini la kunadi nyumba zake.
Shule yake ya Bakili Muluzi ilikuwa hatarini kuuzwa pamoja na nyumba zake zilizo Mbezi Beach.
No comments:
Post a Comment