JK aweka mkakati kuepusha machafuko nchini Burundi - LEKULE

Breaking

21 Mar 2015

JK aweka mkakati kuepusha machafuko nchini Burundi

Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha Burundi inaendelea kuwa na amani, Rais Jakaya Kikwete ameishauri nchini hiyo kutekeleza mambo manne ili kuepuka kuingia katika machafuko ya kisiasa.

Taarifa ya Mawasiliano ya Rais Ikulu iliyotolewa jana, ilisema Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alitoa ushauri huo alipohutubia Bunge la Afrika Mashariki katika Ukumbi wa Bunge la Burundi.

Katika hotuba yake ambayo hutolewa kila mwaka na mwenyekiti wa jumuiya hiyo ilihusu hali ya sasa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyataja mambo hayo kuwa ni wananchi na viongozi wa Burundi kuheshimu kwa vitendo na imani Katiba ya nchi hiyo, makubaliano ya Arusha yaliyozaa amani nchini humo na Sheria za Uchaguzi.

“Viongozi na wananchi wa Burundi kujiepusha na kuvutiwa na matumizi ya nguvu katika kutafuta majawabu ya matatizo yao, jambo ambalo linaweza kuiingiza nchi hiyo katika matatizo makubwa zaidi,” ilisema taarifa hiyo ikimnukuu Rais Kikwete.

“Rais Kikwete amewashauri viongozi na wananchi wa Burundi kutumia mazungumzo na majadiliano, kwa kadri inavyowezekana, akisisitiza kuwa hakuna ukosefu wa watu wenye busara na taasisi ambazo zinaweza kusaidia kusimamia na kuendesha mazungumzo na majadiliano hayo.”

Jambo la nne Rais Kikwete amewashauri viongozi na wananchi wa Burundi wanastahili kufanya katika hali ya sasa ni kutumia Sheria za Burundi inapotokea kuwa baadhi ya wananchi wakahisi kuwa Sheria za Uchaguzi za Burundi zinakiukwa.

“Kwa kaka zangu na dada zangu wa Burundi, pengine niseme kuwa ninatambua wasiwasi kuhusu mchakato wa uchaguzi ambao uko mbele yenu. Kuna minong’ono na hofu kwamba amani na utulivu ambao umekuwepo katika Burundi kwa miaka karibu 15 sasa huenda ikapotea. Wengine wanasema yanaweza hata kuwapo machafuko. Tunaomba Mungu haya yasitokee,” ilisema taarifa hiyo.

“Hivyo, nawaomba viongozi wa Burundi – viongozi wa kisiasa, viongozi wa kidini, viongozi wa kijamii pamoja na taasisi za kijamii kufikiria kufanya yale ambayo nashauri, yanaweza kusaidia nchi yetu hii nzuri, kubakia na utulivu na amani.”

Rais Kikwete alisema: “Tuna imani nanyi kwamba mnao uwezo wa kukabiliana na changamoto za sasa na kuzipatia majawabu. Huko nyuma mmepata kukabiliana na changamoto kubwa zaidi na mkazimaliza. Sioni kwa nini mshindwe zamu hii. Jipeni ujasiri, jipeni utashi wa kisiasa na yote yatakuwa sawa.”

No comments: