Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alizimia na kisha kukimbizwa hospitali wakati akihojiwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Gwajima ambaye alijisalimisha kituoni hapo saa 8:22 jana mchana akiitikia wito wa polisi uliomtaka kufika kutokana na tuhuma za kutoa lugha chafu dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Waandishi wetu waliokuwa kituoni hapo wanaeleza kuwa walimuona Gwajima akitolewa kutoka katika chumba cha mahojiano akiwa amebebwa.
Kwa mujibu wa waandishi hao Gwajima ambaye alikuwa amebebwa na maofisa wa polisi alipelekwa moja kwa moja kwenye gari aina ya Noah kwa ajili ya kumpeleka hospitali.
Tukio hilo lililotokea majira ya saa 3:16 usiku lilikuja katika kipindi kisichozidi dakika saba tangu askofu huyo alipoonekana akiwa ameshikiliwa na wasaidizi wake kuelekea msalani huku yeye mwenyewe akiwa amejishika kichwa.
Wakati akipelekwa hospitali, msafara wake ulikuwa ni wa magari mawili mojawapo likiwa ni aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili PT 1848 na Noah yenye namba za usajili T 215 BEM.
Akizungumza na mwandishi wetu kituoni hapo, mwanasheria wa askofu huyo, John Mallya alisema wakati wakiwa katika mahojiano, alisema anahisi kizunguzungu na baadaye akaishiwa nguvu na akawa amefumba macho.
Mallya alisema baada ya hali hiyo kutokea, polisi walimchukua na kisha kumpeleka katika hospitali ya Jeshi la Polisi iliyoko Kurasini, Dar es Salaam.
Wakati Mallya akiwasiliana na mwandishi majira ya 4:30 usiku alisema kuwa walikuwa wakifanya mchakato wa kumuhamishia katika hospitali ya TMJ kutokana na hali yake kutokuwa nzuri.
“Siwezi kujua tatizo ni nini na siwezi kuzungumza chochote kuhusu hilo maana hayo ni mambo ya kitabibu” alisema Malya.
Ilipotimu saa 4:41 Waandishi wetu ambao nao walifika katika hospitali hiyo ya Jeshi la Polisi walishuhudia Gwajima akitolewa katika hospitali hiyo ya Jeshi la Polisi na kisha kupakizwa katika gari maalum la kubebea wagonjwa lenye namba DFP 6309.
Wakati hayo yakitokea taarifa nyingine zilizotufikia zilidai kuwa; kwa muda wote akiwa katika mahojiano, Gwajima alikuwa hajala chochote hali ambayo iliibua wasiwasi kwamba huenda ilichangia kubadilika kwa afya yake.
Polisi mmoja aliyekuwa katika chumba cha mahojiano aliwaeleza waandishi wetu kwamba Askofu Gwajima alipoteza fahamu muda mfupi baada ya kuhojiwa kuhusu mali anazozimiliki.
Awali wakati Gwajima alipowasili kituoni hapo mchana kabla ya kuhojiwa alizungumza na waandishi wa habari ambapo alikiri kutoa lugha chafu dhidi Kardinali Pengo.
Gwajima ambaye alifika kituoni hapo saa 8:22 mchana alisema kauli yake hiyo ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii aliitoa kutokana na Kardinali Pengo kuwageuka wenzake ambao ni Baraza la Maaskofu Tanzania linalounganisha Wakatoliki, Pentekoste na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kukubaliana kwa pamoja kuwa hawataki Mahakama ya Kadhi.
Alisema maaskofu wote walikubaliana kuhusu tamko hilo na kisha kulisaini lakini anamshangaa Kardinali Pengo ambaye pia alisaini kuwageuka.
“Mimi kama kiongozi wa kiroho nikaona nimkemee kiongozi mwenzangu wa kiroho aache mambo ambayo si mazuri. Hakuna maneno ya kashfa ambayo nimeyatoa. Niliyotoa ni neno la Mungu linalotumiwa kumwongoza mtumishi wa Mungu,” alisema Gwajima.
Alisema anashangaa kuitwa polisi kwani hajatukana polisi na ndio sababu akaitika wito na kufika.
Gwajima alifika polisi akitembea kwa miguu kutokana na foleni kali iliyokuwepo barabarani huku akiwa ameongozana na Mwanasheria wake John Malya pamoja na baadhi ya wachungaji, waumini wa kanisa hilo na wengine waliotajwa kuwa ni walinzi wake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna Suleimani Kova alisema Mchungaji Gwajima ametii amri ya Jeshi hilo kama alivyotakiwa.
Kova alisema baada ya kufika kituoni hapo alielekezwa kwenda kumuona Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam SACP Costantine Massawe.
Akitaja tuhuma zinazomkabili Mchungaji Gwajima, Kova alisema ni pamoja na kumkashifu na kumtukana hadharani kiongozi wa Kanisa Katoliki Kardinali Pengo.
“Taratibu za kuhojiwa zimeshaanza kwa mujibu wa sheria na mtuhumiwa atapewa haki zote anazostahili ikiwemo kuwa na ndugu yake wa karibu, rafiki anayemwamini au wakili wake. Kama ilivyokawaida utakusanywa ushahidi kutoka pande zote za shauri hilo ili kubaini ukweli wa jinsi tukio hilo lilivyotokea,” alisema Kova.
Kova alisema baada ya hapo hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kupata maoni ya kitaalamu na ya kisheria ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka.
“Ili ufanisi upatikane katika upelelezi wa shauri hili ni muhimu kupata ushirikiano kutoka kwa kila atakayetakiwa kulisaidia Jeshi la Polisi kukamilisha haraka upelelezi wa shauri hilo ambalo limepata mvuto mkubwa kwenye jamii,” alisema Kova.
No comments:
Post a Comment