gari hizi, huwaelezi kitu akinadada - LEKULE

Breaking

30 Mar 2015

gari hizi, huwaelezi kitu akinadada





Miaka 20 iliyopita ilikuwa ni nadra kukutana na mwanamke anaendesha gari na wachache waliomudu kuwa na chombo hicho walionekana kuwa na uwezo wa hali ya juu.

Huenda hali hiyo kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na dhana ya mfumo dume uliojengeka katika katika jamii kuwa wanaume ndiyo wanaopaswa kumiliki na kuendesha magari.

Dhana hiyo ilianza kuondoka kuanzia miaka ya 2000 baada ya wanawake wachache kuamua kuvunja ‘mwiko’ kwa kununua na kuingia barabarani wakiwa na magari yao.

Baada ya mfumo wa uendeshaji gari kubadilishwa kutoka ‘manual’ hadi ‘automatic’, ndivyo idadi ya wanawake waliotaka kuendesha magari ilivyoongezeka.

Anael Kimario ambaye anajihusisha na biashara ya uagizaji wa magari kutoka nje ya nchi anasema hivi karibuni idadi ya wanawake wanaoendesha vyombo hivyo imeongezeka maradufu.

Anasema pamoja na kuendesha wanawake pia wamekuwa na uthubutu wa kumiliki magari tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo chombo hicho kilikuwa kinaonekana cha anasa.

“Mambo yamebadilika wanawake wamekuwa na uthubutu wa hali ya juu kutaka kumiliki na kuendesha magari na ndiyo maana ukipita barabarani haiwezekani ipite dakika mbili bila kumuona mwanamke kwenye usukani.”

Kimario anaeleza kuwa ujasiri huo wanawake umechangiwa kwa kiasi kikubwa wa utengenezaji wa kisasa unaofanya zoezi zima la uendeshaji gari kuwa rahisi.

“Unajua magari mengi kwa sasa yamerahisishwa teknolojia yake yanakuwa automatic hivyo kwa kiasi kikubwa linajiendesha lenyewe kwa msaada mdogo wa dereva ndiyo maana wanawake wengi wanaweza kuendesha bila wasiwasi wowote”

Magari gani yananunuliwa zaidi na wanawake kwa sasa?

Kimario anaeleza kuwa licha ya wanawake wengi kumiliki magari lakini idadi kubwa ya magari hayo huwa ni yale yanayouzwa na kuendeshwa kwa gharama nafuu.

Anataja Toyota IST kuwa ni mojawapo ya aina ya gari ambayo inanunuliwa zaidi na wanawake kwa sasa tangu kuanza kuingizwa nchini miaka mitatu iliyopita.

Gari hili ambalo bei yake ni kati ya Sh9 milioni na Sh12 milioni limekuwa kivutio kikubwa kwa wanawake kutokana na muundo wake wa nje.

Udogo wa ‘engine’ ya gari hilo umechangia kuwavutia wanawake wengi kwani inatumia kiwango kidogo cha mafuta hali inayowawezesha wengi kumudu gharama za uendeshaji.

Kimario analitaja gari lingine linalonunuliwa zaidi na wanawake ni kuwa ni Toyota Spacio modeli mpya ambalo umbile lake ni kubwa kidogo ikilinganishwa na IST.

“Spacio bei yake inaanzia kwenye milioni 10 mpaka 15, gari hili linawavutia wengi kutokana na muundo wake wa nje upo kama yai halafu ni imara endapo mtumiaji atakuwa muangalifu,” anasema Kimario.

Kwa upande wake Hubert Muganyizi ambaye pia hujihusisha na biashara hiyo anasema magari madogo aina ya Toyota Vitz, Raum na Passo yamekuwa yakinunuliwa kwa wingi na wanawake ikilinganishwa na aina nyingine.

Muganyizi anaeleza kuwa sababu ya magari hayo kuwa na soko kubwa kwa wanawake inatokana na unafuu katika bei ya ununuzi na gharama za uendeshaji.

“Kwanza magari haya yanauzwa bei nafuu mfano Passo na Vitz inacheza kwenye milioni saba mpaka tisa na ukiagiza kutoka Japan inakuwa nafuu halafu kitu kingine ni miundo yake inaendana kabisa na wanawake,” anasema Muganyizi.

Anasema, “Sina kumbukumbu vizuri lakini mzigo wa magari nilioagiza mwishoni mwa mwaka jana nililazimika kuongeza idadi ya Passo, Vitz na IST kwani zimekuwa zikihitajika zaidi na wateja wa jinsia zote.”

Pamoja na unafuu wa bei, Muganyizi anasema upatikanaji wa vipuli vya magari hayo kwa urahisi ni sababu nyingine inayochangia kupendwa siyo na wanawake pekee bali watu wengi wa hali ya kawaida kiuchumi.

Anaeleza kuwa magari aina ya Toyota RAV 4 na Nadia nayo yamekuwa yakipendelewa zaidi na wanawake lakini idadi yake siyo kubwa ikilinganishwa na magari madogo.

Vitu gani wanaangalia wanawake wanapochagua gari?

Brenda Maganga anasema kabla ya kufanya uamuzi wa kununua gari analomiliki kwa sasa ambalo ni Toyota Spacio alizingatia mambo kadhaa lakini kubwa lilikuwa rangi na unafuu katika gharama.

“Chaguo langu la kwanza lilikuwa aina ya gari pili ilikuwa rangi masuala ya kiufundi siyafahamu kwa sana ingawa kwa akili ya kawaida naweza kubaini kuwa hari haliko sawa,” anasema Brenda.

Kwa upande wake Lilian Kisamo jambo kubwa analozingatia kwenye uchaguzi wa gari ni ukubwa wa mashine na ulaji wake wa mafuta.

“Kwa hali ya maisha ya Watanzania wengi tunaangalia gharama binafsi lazima nichague gari zuri ambalo litakuwa na bei nafuu halafu hata uendeshaji wake nitaumudu hivyo napendelea gari linalotumia mafuta kidogo”

Takwimu hizo haimaanishi kuwa ni aina hizo za magari pekee ndiyo hununuliwa na wanawake Kimario analeza wapo wanaonunua magari yenye gharama na muundo mkubwa kama ilivyo kwa wanaume. Anayataja Toyota Allex, Runx, Harrier ni aina nyingine za magari ambazo zimekuwa zikipendwa na kununuliwa na wanawake.

“Wapo wanawake wanaonunua magari ya kifahari kama Range, Prado, VX, Kluger, Alteza, Mark X, Verossa, Voxy, Lexus lakini hawa siyo wengi kama ilivyo kwenye magari madogo niliyokueleza,” anasema Kimario.

No comments: