JESHI la Polisi mkoani Tanga, limedai kufanikiwa kumkamata mmoja wa
watuhumiwa aliyehusika kwenye tukio lenye sura ya kigaidi katika mapango
ya Amboni.
Zaidi Jeshi hilo limemuhusisha mtuhumiwa huyo na tukio la uporaji silaha
kwa askari waliokuwa doria eneo la barabara ya nne na tano Mtaa wa
Makoko jijini Tanga, Januari 26 mwaka huu.
Takribani mwezi mmoja uliopita, tukio hilo la Amboni ambalo msingi wa
kujulikana kwake ulitokana na kuporwa kwa silaha hizo, lilisababisha
mapambano makali ya kurushiana risasi kati ya polisi wakishirikiana na
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya watu hao
wanaosadikiwa kuwa majambazi au magaidi waliokuwa wamejificha katika
mapango ya Amboni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Tanga, Juma Ndaki, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Machi 18 mwaka huu
saa mbili usiku katika eneo la Kabuku huku akiwa na bunduki yenye
risasi 29.
Ndaki alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kumekuja baada ya jeshi hilo kupata taarifa za siri kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo walimuhoji ambapo mbali na
kukiri kuhusika katika kupora silaha, pia alikiri kuwa ni miongoni mwa
wanaounda kundi hilo lililokuwa limejificha katika mapango hayo yaliyoko
katika Kijiji cha Mleni.
Kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa huyo alikiri kuwapo ndani ya mapango
hayo wakati wa mapambano baina yao na Jeshi la Polisi na kwamba alikuwa
ni mtu wa mwisho kutoka katika mapango hayo akiwa na bunduki moja
iliyokuwa imefichwa.
Kaimu
Kamanda huyo alisema Machi 19 mwaka huu baada ya mtuhumiwa huyo
kukamatwa, saa mbili asubuhi aliwaongoza askari wa kikosi kazi
Taifa wakiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Tanga (RCO)
kwenda kuwaonyesha silaha hiyo.
Alisema baada ya kufika katika mapango hayo walionyeshwa bunduki moja
aina ya SMG yenye namba 14303545 ikiwa na risasi 29 ambayo ni miongoni mwa silaha zilizoporwa askari Januari 26 mwaka huu.
Alisema mtuhumiwa huyo pia aliwaonyesha panga moja, begi moja la
kahawia likiwa na nguo mbalimbali na mabomu matatu ya kutengeneza
kienyeji vifaa ambavyo walikuwa wakivitumia wakati wa mapambano kati yao
na polisi waliokuwa wakisaidiwa na JWTZ.
Aliongeza kuwa kupatikana kwa silaha hiyo kunafanya silaha zote mbili
walizoporwa askari wa Jeshi hilo ambao walikuwa doria kupatikana.
No comments:
Post a Comment