Elimu ndiyo silaha ya mwanamke - LEKULE

Breaking

17 Mar 2015

Elimu ndiyo silaha ya mwanamke

“Bidii, kujiamini ndiyo silaha pekee, mimi sikuogopa kukimbilia fursa nilikuwa na ujasiri kwani ukweli sikujilipia mwenyewe elimu ya chuo kikuu nchini Uingereza, bali nilipata ufadhili. Namshukuru mama yangu alinifunza kujiamini kwani hata yeye alikuwa akijiamini sana ndiyo maana alitulea bila kutetereka,”. Ndivyo anavyoanza kusema Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya Multi Choice Tanzania, Barbara Kambogi.
Barbara aliyezaliwa mjini Muheza mkoani Tanga Juni 1983, anasema haikuwa kazi rahisi kufikia hatua aliyopo sasa, bali alifanikiwa kutokana na kujiamini sambamba na elimu aliyopewa na mama yake mzazi kuhusu maisha na njia za kufanikiwa.
“Nyumbani kwetu tulizaliwa wawili na dada yangu Nancy, baba yangu alifariki baada tu ya mimi kuzaliwa. Kwa kuwa mama yetu alikuwa amesoma alihamia nchini Kenya alikokuwa akifanya kazi katika Shirika la Unilever akiwa Katibu Muhutasi Mkuu, huko nilisoma chekechea mpaka darasa la tano, kabla mama yangu hajarudi Tanzania,” anasema Barbara.
Hata hivyo, Babra anasema alilazimika kuhamia nchini Zimbabwe ambako mama yake mdogo alikuwa akiishi mjini Harare ambako alimalizia darasa la saba na kupata ufaulu wa juu alama ya nane. Katika Shule ya Courteney Selum.
Barbara anasema baada ya kukamilisha elimu yake nchini Zimbabwe, safari hii alirudi nyumbani na kujiunga kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya St Anthony Mbagala. Hata hivyo, alikwenda kumaliza kidato cha sita katika Shule ya Street Swaminarayan Academy iliyopo Mombasa nchini Kenya.
“Baada ya kuhitimu sikuwa na chaguo wakati bado nafikiria, yakaja matangazo vyuo ya nje wanatafuta wanafunzi, nikajipa moyo kushiriki nikafanikiwa kuchaguliwa katika Chuo Kikuu cha Glamorgan kilichopo Jiji la Cardif nchini Uingereza.
Nilichagua kusomea ‘Media Communication’ kwa miaka mitatu, nilifaulu mzuri. Nikafikiria na kuamua ni heri nimalize elimu yangu, nikaamua kusoma shahada ya pili katika mchepuo wa ‘Public Relation’ katika chuo cha Cardif University ambacho ni kati ya vyuo bora saba duniani.
“Sitaisahau Januari 19, 2009 nilipopigiwa simu na mwalimu wangu kutaarifiwa kuwa nimepata ufaulu mzuri hivyo nitahitimu shahada ya uzamili,” anasema Barbara.
Akizungumzia namna alivyopata kazi Multi Choice Tanzania, Barbara anasema alipohitimu alifikiria kufanya kazi nchini mwake, japokuwa alikuwa na mawazo mengi na kufanya kazi kadhaa nchini Uingereza, aliona tangazo la ajira ya Meneja Mawasiliano na Uhusiano Multi Choice iliyokuwa imeachwa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu na Lucy Kihwele.
“Nilituma maombi Agosti 2009 na kufanikiwa kuitwa katika usaili. Nilifanya usaili na kuondoka kurudi Uingereza, nikiwa huko nilipokea barua pepe kuwa nimefanikiwa kupata nafasi hii, nilifungasha virago vyangu na kurudi nchini, ambako tangu nipate nafasi hii sijawahi kuondoka hapa.”
Barbara anasema japokuwa wanawake wanahitaji usawa, mtu haamki asubuhi na kupata nafasi aliyonayo, bali inahitaji kujituma katika kuandaa mazingira ili kuweza kuzitumia nafasi zinazojitokeza.

Akizungumzia kazi na maisha yake binafsi, Barbara anasema katika utendaji wake hajawahi kuchanganya kazi na masuala yake binafsi, kwani anaamini kwa kufanya hivyo atawapa watu nafasi ya kumjadili katika mambo yasiyofaa ilhali yeye ni kioo cha jamii.

“Ukiwa mwanamke ambaye unatokea katika vyombo vya habari na maeneo mengine yenye makundi makubwa ya watu, unapaswa kuwa makini sana, ila nashukuru sijakumbwa na dhahama. Uzuri ni kwamba napangilia mambo yangu kama kazi za usiku na hata kusafiri,” anasema na kuongeza:

“Mimi ni mke, naenda sokoni, napika, nafua na kufanya shughuli zote za nyumbani mwenyewe. Napanda daladala, bajaji lakini si bodaboda hizo naogopa sana kwakuwa si salama,” anasema Barbara huku akicheka.

Anasema kazi aliyonayo imemnufaisha kwa kumpa marafiki wengi, kufahamiana na watu maarufu na wakubwa hapa nchini, licha ya kumpa nafasi ya kutembelea nchi mbalimbali.

“Sikuwahi kuamini kama ningekuja kutembelea nchi maarufu kama Mauritius, lakini kupitia kazi niliyonayo imewezekana na nimejifunza mengi nikiwa huko, pia napata nafasi ya kuendeleza elimu yangu kwa kozi fupifupi na semina kutoka nchi mbalimbali,” anasema.

Hata hivyo, Barbara anasema changamoto si nyingi katika kazi yake, bali vyote vinavyokuja mbele yake anavitumia kama chachu ya kukua.

Akizungumzia familia Barbara ambaye ni mcheshi, anasema ana mume Mkenya aliyekutana naye nchini Uingereza na kusoma pamoja, ambapo alipotaka kurudi nyumbani alimvisha pete ya uchumba na miaka iliyopita walikufunga ndoa.

“Yeye anafanya kazi Kenya Airways, tunaishi nchi tofauti ila tunakutana kila wikiendi, maisha ni mazuri na sioni utofauti kwani ananiunga mkono na ananijali. Muda mwingi nikiwa sipo naye nautumia katika kutembelea watoto yatima na kuwapa misaada, hata akiwepo huwa nafanya hivyo pia ndiyo faraja yangu,” anasema Barbara na kuweka wazi kwamba hajafanikiwa kupata mtoto.

Alisema anapenda sana kula nyama ya ng’ombe na si kuku wala samaki ingawa anajitahidi kufanya mazoezi ili asinenepa kupita kiasi.

No comments: