BONDIA nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka aliyehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela pamoja na faini ya shilingi milioni moja, hapo Februari 2 mwaka huu mjini Morogoro, amebadilishiwa adhabu hiyo na badala yake atatumikia kifungo cha nje.
Cheka alihukumiwa kwa kosa la kumpiga na kumsababishia maumivu makali, meneja wa baa yake ya Vijana Social Hall iliyopo mjini Morogoro, aitwaye Bahati Kibanda, hapo Julai 2 mwaka jana katika eneo la Sabasaba.
Cheka anayeshikilia mkanda wa WBF alipandishwa Kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, kwa shitaka hilo lililosomeka kuwa ni la shambulio la kudhuru mwili na kujeruhi.
Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya mkoa wa Morogoro Said Msuya, aliyesikiliza shauri hilo, alikubaliana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na kuthibitisha shitaka hilo.
Pamoja na Cheka kupewa nafasi ya kujitetea, bondia huyo hakutoa maelezo yoyote na kuiachia mahakama hiyo kutoa adhabu inayostahili kwa bondia huyo aliyejizolea sifa kemkem katika ngumi za kulipwa nchini.
Hata hivyo, taarifa kutoka Morogoro zinasema kuwa Cheka ameachiwa kutoka katika gereza la Manispaa ya Morogoro, mchana wa leo na kwamba sasa atatumikia kifungo cha nje, sambamba na kumlipa fidia ya shilingi milioni moja meneja wake huyo wa zamani.
Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Cheka atatakiwa kuripoti katika gereza la Manispaa ya Morogoro kila wiki, hatakiwi kutoka nje ya Manispaa ya mkoa bila kibali maalum cha Gereza na kwamba kwa muda wote huo, atatakiwa kutofanya kosa lolote la jinai, vinginevyo adhabu yake itarejeshwa au kuongezwa.
Kocha wake wa muda mrefu, Abdalah Komando akiwa na wanafamilia ya bondia huyo mjini Morogoro, wamethibitisha kuachiwa kwa mpiganaji huyo, baada ya kukaa gerezani kwa muda wa siku 44.
Habari kutoka mji kasoro bahari zinasema kuwa kulikuwa na shamra shamra kubwa nyumbani kwa bondia huyo, mtaa wa Kilimahewa kwani ndugu, jamaa na marafiki walifurika kwa wingi kumpa pole na pongezi bondia huyo asiye na mpinzani kwa sasa nchini.
Mwandishi wa mtandao huu ambaye alifika nyumbani kwa bondia huyo na kukutana naye wakati akitoka kuoga, alisema baada ya kusalimiana naye kama rafiki, kocha wake alimuomba kumuacha mwanandondi huyo ili apate mapumziko kwa siku nzima ya leo.
Kocha wake huyo, Komando, alisema Cheka bado akili yake haijakaa sawa, hivyo ni vyema kama ataachwa kwa leo ili apumzike, lakini akawahakikishia wanahabari kuwa watapata fursa ya kuzungumza naye mambo mbalimbali kesho.
No comments:
Post a Comment