Uongozi wa Azam FC umesema haujamzuia mshambuliaji wake wa kimataifa, Didier Kavumbagu kurejea kwao kuitumikia timu yake ya taifa ‘Entamba Murugamba’.
Jaffar Idd Maganga, msemaji wa Azam FC, ameuambia mtandao huu kuwa Kavumbagu yuko Tanzania kwa sababu ya uzembe wa Shirikikisho la Soka Burundi.
Amesema kuwa shirikisho hilo liliwasiliana na uongozi wa Azam FC likimuomba Kavumbagu kwa ajili ya kuitumikia timu yake ya taifa katika mechi ya kirafiki ya kalenda ya FIFA mwishoni mwa wiki hili tangu wakiwa Khartoum, Sudan wakicheza dhidi ya El-Merrikh, lakini mkali huyo wa mabao amekwama kwenda kutokana na kutotumiwa tiketi ya ndege.
“Tumeshangazwa na taarifa zinazoenezwa kwamba tumemzuia Kavumbagu kwenda kuitumikia timu yake ya taifa. Hii tunaona imelenga kutuchafua kimataifa.
“Tulipata taarifa za Kavumbagu kutakiwa na timu yake ya taifa tukiwa Sudan, lakini ameshindwa kwenda kwa sababu hajatumiwa tiketi.
“Mchezaji anaruhusiwa na klabu yake kwenda kuitumikia timu ya taifa pale shirikisho linapokuwa limetuma tiketi kwa klabu husika. Tiketi ya Kavumbagu kwenda kuitumikia timu yake ya taifa si jukumu la Azam FC,” amesema Maganga.
Kavumbagu, mchezaji wa zamani wa Atletico FC ya Burundi na Yanga SC, ameifungia Azam FC mabao 10 katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu ikiwa ni bao moja nyuma ya kinara, Simon Msuva wa Yanga SC.(AI)
No comments:
Post a Comment