APPT Maendeleo: Tutamsimamisha mgombea mwanamke urais 2015 - LEKULE

Breaking

30 Mar 2015

APPT Maendeleo: Tutamsimamisha mgombea mwanamke urais 2015



Mwenyekiti wa Chama cha APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray amesema chama chake kitamsimamisha mwanamke kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Mziray ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, alisema wiki iliyopita kuwa mchakato wa kumpata mgombea huyo ndani ya chama, umeanza.

Alisema ingawa  chama hicho kina wanachama wengi wanaume na ambao wana sifa na uwezo wa kuwania nafasi hiyo, anaamini  kuwa mwanamke anayo nafasi nzuri na kubwa kufanya vizuri katika uchaguzi huo.

“Mimi pia nina sifa na hata uchaguzi uliopita niligombea na kushika nafasi ya nne, baada ya aliyekuwa mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba… lakini sasa tumeamua tutoe fursa kwa mwanamke.”

Mziray alisema chama chake kina rekodi ya kuwasimamisha wanawake, akitolea mfano wa uchaguzi wa mwaka 2005 walipomsimamisha Anna Senkoro. Alisema kwa tukio hilo, chama hicho kilijijengea heshima kubwa katika jamii na miongoni mwa wanawake.

“Tulipomsimamisha mgombea huyo, wanawake walituunga mkono, lakini wakasema hakuwa ameandaliwa na wanawake... Sasa tuwepanua wigo, tumewakaribisha wanawake wamuandae mtu wao mwenye sifa, sisi tutamkaribisha na kumuunga mkono, tunaamini wanawake wanaweza na tunawaunga mkono katika jitihada zao” alisema.


Alisema katika utafiti walioufanya kwa muda, wamegundua kuwa wanawake wanao ushawishi mkubwa na wamekuwa katika nafasi nzuri ya kuungwa mkono kutokana na kuwa na maadili na umakini katika uongozi kulinganisha na wanaume walio wengi. “Ukiangalia matukio yote ya ufisadi yanayotokea nchini yanawahusisha wanaume, hata kama yupo mwanamke unakuta ni mmoja au wawili tu… hii pekee inatoa picha ya jinsi wanawake wanavyoweza kutumikia wananchi kwa uadilifu wakipewa nafasi ikilinganishwa na wanaume,” alisema.

Akizungumzia utaratibu wa kumpata mgombea wa chama hicho, Mziray alisema mkutano mkuu wa chama ndiyo utakaokaa na kumpitisha, baada ya kuwachuja na kumpata mmoja mwenye sifa na vigezo vinavyokidhi haja.

“Mkutano mkuu wetu utafanyika tukiwa tayari tunao wagombea wetu, ningependa chama hiki kikamatwe na kina mama…. hatutampata mgombea kwa njia ya kura za maoni, tunapiga vita kura za maoni, zinagawa chama. Tutampata mgombea wetu kwa kuzingatia muafaka,” alisema.

Mziray alisema mbali na mgombea urais, chama chake kitasimamisha wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani nchi nzima na wamejipanga kushinda majimbo na kata kadhaa nchini.

“Tumeanza kuwaandaa wanachama wetu na tutahakikisha tunasimamisha wagombea nchi nzima…. tunawakaribisha Watanzania wasiopenda mizengwe, hawana haja ya kusubiri mgombea binafsi, waje APPT-Maendeeleo huku hakuna migogoro,” alisema.

Alisema chama hicho kimejenga ngome yake katika maeneo ya Same, Musoma na  Kigoma.

No comments: