Anglo Leasing:viongozi washtakiwa Kenya - LEKULE

Breaking

4 Mar 2015

Anglo Leasing:viongozi washtakiwa Kenya

Maafisa wakuu wa serikali ya Kenya wakiwemo mawaziri na makatibu wa kudumu wamefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka kuhusiana na kashfa ya anglo leasing iliyogharimu serikali ya kenya mabilioni ya madola, miaka kumi iliyopita.

Maafisa hao saba ni miongoni mwa wanasiasa mashahuri na wafanyabiashara wanaodaiwa kulaghai serikali ya kenya kupitia kandarasi ghusi.

Hata hivyo washukiwa hao walikanusha madai hayo na kuachiliwa kwa dhamana.

Aliyekuwa waziri wa fedha wa Kenya Chris Obure ambaye sasa ni seneta wa kisii, makatibu kadhaa wa kudumu katika wizara ya usalama wa ndani na fedha.

Joseph Magari, Sammy Kyungu na Dave Mwangi ni miongoni mwa waliofikishwa mahamani kujibu mashtaka.

Wengine ni pamoja na Francis Chahonyo, aliyekuwa mkurugenzi wa kampuni ya Posta, Samuel Bundotich, katibu katika wizara ta fedha na mkuu wa masuala ya madeni katika wizara hiyo David Onyonka.

Waziri mwingine wa zamani wa fedha David Mwiraria ambaye pia ni miongoni mwa washukiwa hakufika mahamani, wakili wake alifahamisha mahakama kuwa mteja wake amelazwa katika hospitali moja mjini Nairobi, na hivyo kuomba mahakama kusubiri hadi atakapopona.

Mfanya biashara maarufu Deepak Kamani, babake Chamanlal Kamani, nduguye Rashmi na wawakilishi wa kampuni mbili zilizohusishwa na kashfa hiyo hawakufika mahakamani.

Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko, alifahamisha mahakama kuwa watatu hao wanatarajiwa kuwasili nchini leo usiku na kesho watafika mbele ya tume ya kupambana na ufisadi kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Wakili wa mfanyabiashara huyo Ahmed Nassir aliiambia mahakama hiyo kuwa watatu hao hawana nia ya kukwepa kufika mahakamani.

Washukiwa hao saba waliofika mahakamani walikanusha mashtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana hadi tarehe kumi na nane mwezi huu wakati kesi hiyo itakaposikilizwa.

Hata hivyo mahakama imeagiza washukiwa hao kuwasilisha pasi zao za usafiri mahakamani na kuonywa dhidi ya kusafiri nje ya nchi bila idhini ya mahakama.

Washukiwa wengine wawili Bradley Beckenfeild ambaye anasemekana kuishi nchini Marekani na Brian Mills ambaye hajulikani aliko hawakufika mahakamani.

Mkurugenzi wa mashtaka Keriako Tobiko ameiomba mahakama hiyo kutoa kibali cha kimataifa cha kukamatwa kwao ili wafikishwe mahakamani.

Wote walikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya dola elfu kumi na moja za kimarekani.
Aidha mahakama iliamrishwa raia wawili wa kigeni wanaohusishwa na sakata hii kukamatwa.
Sakata ya Anglo Leasing ilitokana na zabuni mbovu za serikali, zilizodhamiria kuweka mitambo mpya za kutengeneza passpoti pamoja na vifaa vya kisasa vya Kiusalama.
Zabuni hiyo kwanza ilipewa kampuni ya Kifaransa, kabla ya nia kubadilika na kampuni ya Uingereza kuipata, huku bei zikiwa zimepandishwa mno.
Inasadikika kuwa Kenya imepoteza takriban dola bilioni moja kupitia sakata hii

No comments: