STAA wa muziki wa kizazi kipya Bongo, Ally Saleh ‘Ali Kiba’, amefunguka mengi kuelekea katika shoo anayotarajiwa kufanya Aprili 5, mwaka huu ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem, Dar
Hii itakuwa ni mara nyingine kwa msanii huyo kupanda jukwaani hapo baada ya kufanya hivyo miaka miwili iliyopita na sasa mashabiki wanamsubiria kwa hamu kumuona kipenzi chao akikamua ngoma zake kali zikiwemo, Kimasomaso, Mwana Dar es Salaam, Single Boy, My Everything na nyingine kibao bila ya kuusahau mkwaju mpya unaojulikana kwa jina la Chekecha Cheketua.
Staa huyo ambaye kwa sasa anatamba na ngoma hiyo ya Chekecha Cheketua alifanya mahojiano na Mikito Jumatano akielezea kwa ufupi alivyojipanga na kazi zake za kimuziki.
Wimbo wa Chekecha Cheketua ni maalum kwa nani?
Kama mashabiki wengi wa muziki walivyozoea kuona msanii akitoa wimbo huwa unamlenga mtu fulani iwe kwa mazuri au mabaya, lakini imekuwa tofauti kwa Ali Kiba ambaye anasema wimbo wake mpya ameutoa kama bidhaa miongoni mwa bidhaa zake.“Ninahisi wasanii tunatofautiana sana, nimetoa wimbo huu kama kazi tu, yaani ni miongoni mwa bidhaa yangu mpya ambayo itabamba vilivyo pale Dar Live.”
Baada ya Chekecha Cheketua tutarajie nini?
Imekuwa ‘fasheni’ kwa baadhi ya wasanii kutoa nyimbo mfululizo kwa lengo la kuwafanya mashabiki wao kuwasikia tofauti kwa kipindi kifupi, kwa upande wa Ali Kiba ambaye hukaa kimya kwa kipindi kirefu na akija hutoa mikwaju ya ukweli inayoteka hisia za mashabiki, anasema; “Tusubiri kwanza tuone mashabiki wataipokeaje hii ngoma na matokeo yatakavyokuwa ndiyo mipango ya kutoa nyingine itafuata kama itapokelewa vizuri itanipa nguvu zaidi.”
Mipango yako kwa sasa
“Nimejipanga vizuri na mashabiki wangu popote walipo watarajie mapinduzi ya muziki kutoka kwangu, ninawaahidi sitawaangusha kwa kuwa najua wanataka burudani safi.”
Huyo ndiyo Ali Kiba ambaye amefunguka machache aliyonayo kuelekea katika shoo ya Sikukuu ya Pasaka, Aprili 5, mwaka huu. Mbali na Kiba, siku hiyo watapanda wasanii kibao jukwaani akiwemo Mfalme wa muziki wa Kigodoro Bongo, Msaga Sumu, Mkali wa mambo ya Pwani, Isha Mashauzi akiwa na kundi lake la Mashauzi Classic.
Kwa mashabiki wa burudani nchi nzima hakika hii siyo shoo ya kukosa kwa kuwa kila mmoja anaangalia nini kinachoweza kutokea hapa, hakika itakuwa siku safi kwa wanaburudani.
No comments:
Post a Comment