Huduma za kutuma na kupokea fedha na kufanya mihamala mbalimbali ya
malipo zinazotolewa na makampuni ya Vodacom Tanzania kupitia huduma yake
ya M-Pesa na Tigo kupitia huduma yake ya Tigopesa zitazidi kuimarika
kutokana na makampuni hayo kuingia makubaliano ya kutoa huduma hizo kwa
ushirikiano.
Ushirikiano huo utawawezesha wateja wa makampuni hayo kutuma na kupokea fedha na kufanya mihamala ya malipo moja kwa moja.
Makubaliano hayo ambayo yametangazwa jana yatawawezesha mamilioni ya
wateja wanaotumia huduma za M-Pesa na Tigopesa kupata huduma kwa ubora
zaidi kwa kuwa mteja akipokea au kutaka kutuma pesa au kufanya malipo
hatolazimika kutoa fedha kwenye mtandao mmoja kwenda mwingine kama
ilivyo sasa bali atafanya akitakacho moja kwa moja na bila kutozwa
malipo ya ziada.
Akiongea jana wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza alisema “Haya ni mapinduzi makubwa katika kutoa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi nchini Tanzania. Katika siku za karibuni wateja wa makampuni haya mawili wataweza kutuma na kupokea fedha na kufanya mihamala ya malipo mbalimbali moja kwa moja bila kulazimika kuzitoa kwa mawakala kwanza na kuziingiza kwenye huduma ya fedha ya mitandao yao kama ilivyo sasa.”
Wateja wa M-Pesa hivi sasa wanaweza kulipia huduma mbalimbali baadhi
yake zikiwa ni kulipia ving’amuzi vya televisheni zao, nauli za usafiri
wa ndege, huduma za bima, huduma za maji na umeme, kodi mbalimbali za
serikali, karo za shule, kurejesha mikopo katika mabenki na uchangiaji
katika mifuko ya pensheni.
“Huduma hizi hivi sasa zinatumiwa na watu wengi na kwa kipindi cha miaka saba tangu zianzishwe zimeleta mapinduzi na kurahisisha maisha ya Watanzania kwa kiasi kikubwa. Tuna imani kwa kushirikiana na Tigo katika huduma hii tutanufaisha wateja wa makampuni haya mawili kwa kiasi kikubwa na hivi sasa tuko katika mchakato wa kuboresha mfumo wetu wa M-Pesa ili ifikapo mwisho wa mwaka tutakapoanza kutoa huduma hizi pamoja kusiwepo na matatizo yoyote ya kimtandao na tutawekeza kiasi cha shilingi Bilioni 150/-kwa kazi hii,” alisema.
Meza aliongeza kuwa kushirikiana kwa makampuni haya mawili katika
kutoa huduma za pesa hakutaongeza gharama kwa watumiaji wa Tigopesa na
M-Pesa bali kutawarahisishia kupata huduma bora na kwa karibu kutokana
na mtandao mkubwa wa makampuni haya mawili yanayotoa huduma za
mawasiliano nchini.
“Tunachofanya hivi sasa ni makampuni haya kujipanga kuhakikisha
yatakapoanza kutoa huduma za kifedha kwa pamoja mwishoni mwa mwaka huu
yanatoa huduma za uhakika. Mtandao wetu wa mawakala 85,000 wa M-Pesa
kwa sasa unahudumia zaidi ya wateja milioni 7 ambao wanafanya shughuli
mbalimbali zinazochangia kukua kwa uchumi wa Taifa na tumejipanga
kuhudumia wateja wengi zaidi kwenye miaka ya mbele,” alisema Meza.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo,Diego
Gutierrez alisema ushirikiano huu utawanufaisha wateja wengi wa
makampuni haya mawili na kuwarahishia maisha na kuwawezesha kufanya
biashara zao vizuri wakati huo huo fedha zao zikiwa salama
“Tuna imani kwa kushirikiana na Vodacom katika huduma hii
tutanufaisha wateja wa makampuni haya mawili kwa kiasi kikubwa na
tutahakikisha wateja wetu wanaendelea kupata huduma bora za kifedha kwa
njia ya mtandao bila kuingia gharama ya ziada na tuna uzoefu wakufanya
kazi katika ushirikiano kama huu kwa kuwa tayari tunashirrikiana na
makapuni ya Airtel na Zantel na wateja wetu wanaendelea kufurahia huduma
nzuru.Tunashukuru Benki Kuu ya Tanzania na Taasisi ya IFC kwa
kufanikisha utaratibu huu wa makampuni haya kutoa huduma kwa pamoja,”
alisema Gutierrez.
Huduma za M-Pesa na Tigo Pesa kwa sasa zinatumika kulipia huduma
mbalimbali baadhi yake zikiwa ni kulipia ving’amuzi vya televisheni zao,
nauli za usafiri wa ndege, huduma za bima, huduma za maji na umeme,
kodi mbalimbali za serikali, karo za shule, kurejesha mikopo katika
mabenki na uchangiaji katika mifuko ya pensheni.
Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC) limekuwa likiunga mkono
kuimarishwa kwa huduma hizi za fedha kwa njia ya simu na hicho ndicho
chanzo cha makampuni haya kuingia makubaliano ya kuunganishwa kwa huduma
hizi nchini Tanzania ili kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wake.
No comments:
Post a Comment