Ugiriki kuwasilisha orodha ya mageuzi ya kiuchumi - LEKULE

Breaking

23 Feb 2015

Ugiriki kuwasilisha orodha ya mageuzi ya kiuchumi


 Iwapo serikali ya Ugiriki inayoongozwa na waziri mkuu Alexis Tsipras itashindwa kuwashawishi wakopeshaji wake wakuu, muda wa kupewa afueni utakamilika Jumamosi hii na serikali hiyo mpya iko katika hatari ya kuishiwa fedha, kuyumba zaidi kwa masoko yake na hata kuondoka kutoka kanda inayotumia sarafu ya euro.

Ijumaa iliyopita,Ugiriki ilipata afueni baada ya waziri wa fedha Yanis Varoufakis kufikia makubaliano na mawaziri wenzake wa fedha wa nchi wanachama 18 wa kanda inayotumia sarafu ya euro kwa kurefushiwa muda wa kuyalipa madeni yake kwa miezi mingine minne.

Hata hivyo makubaliano hayo yalikuja na masharti kuwa Ugiriki sharti iwasilishe orodha ya hatua itakazochukua kuhakikisha inatimiza wajibu wake wa kulipa madeni bila kukwepa masharti na kujikwamua kiuchumi ifikapo hii leo.

Ujerumani yataka misingi kuheshimiwa

Katika taarifa iliyochapishwa katika gazeti la Ujerumani la Bild hii leo, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema kuwa Ulaya ina nafasi ya kupumua, ila suluhu kamili halijafikiwa na kibarua ni kwa Ugiriki kuhakikisha misingi ya usaidizi inasalia kama ilivyo.

 Kwa upande wake Varoufakis amesema iwapo mapendekezo yao ya marekebisho ya kiuchumi hayatakubaliwa, basi makubaliano yaliyofikiwa siku ya Ijuma yatakufa.
Hapo kesho, halmashauri ya Umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha duniani IMF ambao ndiyo wakopeshaji wakuu wa Ugiriki watayadurusu mapendekezo hayo ya Ugiriki.
Wakiridhika nayo basi muda uliorefushwa kwa Ugiriki kulipa madeni utaendelea kama ilivyopangwa ikisubiri kuidhinishwa na mabunge ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na kama sivyo basi ni hatua moja nyuma ambapo mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro watakutana tena wiki hii.
Tsipras aliingia madarakani mwezi uliopita kupitia chama cha mrengo wa kushoto chenye msimamo mkali cha Syriza na kuahidi kukomesha mpango wa kukaza mkwiji alioutaja kuwa ni fedheha na mzigo kwa nchi yake.


Ugiriki yapania kuwapa raia afueni
Waziri mkuu huyo wa Ugiriki anapanga kutumia afueni hiyo ya kurefushiwa muda wa kulipa madeni kujadili upya mpango wa kuufufua uchumi wa nchi hiyo ambapo kati ya watu wanne Ugiriki, mmoja hana ajira kutokana na mgogoro wa kiuchumi na athari za kubana matumizi.


 Serikali ya Ugiriki ina kibarua kigumu cha kuheshimu makubaliano yake na wakopeshaji wake na kutimiza ahadi zake ilizozitoa kwa raia wakati wa uchaguzi.

Ugiriki imeahidi kutumia kiasi cha euro bilioni mbili mwaka huu kupambana na umasikini unaowakumba maelfu ya familia nchini humo walioathirika na kupoteza ajira, kupunguziwa mishahara na kuongezwa kwa kodi

No comments: