Sheria: Namna ya Kuwashitaki Askati Wanaowabambikiza Kesi Raia - LEKULE

Breaking

26 Feb 2015

Sheria: Namna ya Kuwashitaki Askati Wanaowabambikiza Kesi Raia

 Hapa kwetu Tanzania  habari ya kubambakiziana kesi ni kama mtindo. Mara nyingi matendo haya yamekuwa yakifanywa na watu wenye uwezo  kifedha dhidi ya wasio na fedha  pia kati ya  maofisa wa polisi na raia.

Mtu kwasababu ana pesa au cheo anaweza kuamua  kumfungulia yeyote mashtaka.  Watu wengi wako magerezani kwa kubambikizwa kesi, hili wala sio siri tena.

Sisemi walio mahabusu, hao nao hawana idadi. Inasikitisha mno. Ni wazi kuwa wengi wao wamefikia huko aidha kwa kusingiziwa kosa na askari au mtu mwenye cheo au  fedha.

Lakini zaidi wametoka mikononi mwa askari kwakuwa hata huyo mwenye cheo au fedha hawezi kumbambikizia  mtu kesi  bila kupitia kwa askari. Kwahiyo askari  ndio  tatizo  kubwa  katika  hili.

 1.Nini maana ya kubambikizwa kesi.
Kubambikizwa kesi au kumshtaki mtu kwa  hila  maana yake ni kumfungulia mtu kesi ya jinai  bila  mafanikio , na bila sababu za msingi za kufanya hivyo  na mtu huyo  akapata  athari zozote kutokana na kumfungulia kesi hiyo.    

Athari ni pamoja  na kupotezewa muda, gharama, usumbufu, kudhalilishwa, kupata hasara kibiashara au kikazi kutokana na kushikiliwa na kila kitu ambacho kimekuwa kama  matokeo ya kusingiziwa kesi  ni athari kwa maana hii.

2. Sababu za kuwabambikiza watu kesi.
Sababu  za kumuuzia mtu kesi  huwa ni nyingi. Ni  nyingi  kutokana  na kuwa kila aliyebambikizwa  kesi huwa kuna mgogoro nyuma uliosababisha  jambo hilo  na migogoro  kawaida inatofautiana.

Pamoja  na hayo sababu  kuu  za kubambikizia  mtu kesi huwa ni kwa ajili ya kumkomoa  au kulipiza kisasi kutokana na chuki zilizotokana na mgogoro  kama  nilivyosema.

3. Weledi wa Askari wetu na kuwabambikiza raia Kesi.
Wakati  mwingine  askari  wetu  huwabambikizia  watu kesi  katika  mazingira  ya  kushangaza kabisa. Askari  anaweza  kumbambikizia  raia  kesi  kwasababu  tu  raia  amehoji  jambo  fulani.

Kwa mfano mtu anaweza kumuuliza askari nioneshe  kitambulisho  chako kabla  hujanikamata. Utasikia  askari akimwambia  mtu unajifanya  mjuaji tutaona, mara unanifundisha  kazi utanitambua n.k.

 Eti mazimgira kama hayo kwa askari wetu utakuwa tayari  ni mgogoro  na  mtu atapofikishwa  kituoni  basi ni rahisi  kupewa  kesi ambayo si  yake  ilimradi tu askari  aoneshe  kuwa aliposema  utanitambua, utaona  alikuwa  na uwezo  wa kufanya  hivyo  kweli.

4. Athari za kubambikiza watu kesi.
Kwanza upelelezi wa kesi ambayo haipo unagharimu  pesa  za serikali  na muda ambao kimsingi ungetumika kushugulikia kesi nyingine za watu wanaohitaji haki kiukweli.

Pili  kesi hizi za kubambikizwa  zinaongeza idadi ya kesi mahakamani pasi na sababu za msingi na hivyo kusababisha kesi za kweli kuendelea kuchelewa.

 Tatu kesi hizi ni usumbufu kwa waliobambikizwa na ndugu zao na  zinaathiri nguvu kazi katika taifa kwani badala ya watu kuendelea na uzalishaji mali  hubaki kushughulikia kesi hizi zisizowahusu na baadhi yao kufungwa kabisa na hivyo kupoteza moja kwa moja nguvu kazi katika jamii.

 5.Namna ya kumshitaki aliyekubambikiza kesi.
Kushitaki  ninakokuongelea  hapa  ni kushtaki kwa  madai  yaani  kumdai aliyekubambikiza kesi akulipe kutokana na tendo  hilo ovu. Hivyo hii itakuwa  ni kesi  ya madai na hatua  zake  ni  hizi.

( a ) Kwanza inategemea  unataka  akulipe shilingi  ngapi. Kuanzia  shilingi  moja  mpaka  milioni  tano utaenda  mahakama  ya mwanzo. Ukifika hapo mahakamani  utaeleza shida  yako pale na  watakusaidia  kufungua  kesi hiyo.

 Aidha  kuanzia  milioni tano  na kuendelea  mahakama   unayotakiwa  kufungua  kesi  ni ya wilaya  na Mahakama  kuu. Napo ukifika  mahakamani  utaelekezwa  utaratibu  wa kufungua kesi lakini  kwa mahakama  hizi  ni vema ukamuona  mwanasheria  kabla  ya kwenda mahakamani.

( b )Kwa ajili ya kufungua shauri  hilo utaratibu ni mwepesi kihivyo na bila  shaka  baada  ya  kufanya  hayo  utakuwa umefungua  kesi  ya kulipwa  kutokana  na  kubambikizwa.

6.Mambo unayotakiwa kujiandaa nayo ili ushinde kesi ya kubambikizwa..

( a ) Kwanza hakikisha  unatunza makaratasi  yote yanayohusu  ile  kesi  ya  jinai  uliyofunguliwa kwa kubambikizwa. Makaratasi( documents) hayo ndiyo yatakayotumika  kuonesha  kuwa kweli kesi  ya jinai  dhidi yako ilifunguliwa.

( b ) Zingatia  sana  kuwa kubambikizwa  kesi  ni pale  tu unapofunguliwa mashtaka polisi na haijalishi  mashtaka  hayo  yamefika  mahakamani  au hapana. Kitendo cha kufikishwa polisi kwamba umetenda kosa fulani wakati  si  kweli tayari umebambikizwa kesi.

( c ) Pia  kama  ulibambikizwa  kesi  ikafika  mpaka  mahakamani  na ukaachiwa huru hakikisha  unapata  nakala  ya hukumu inayoonesha  kuwa uliachiwa huru kwakuwa itakuwa ushahidi kuwa kesi haikuwa ya kweli na ndio maana  mahakama  iliitupilia  mbali.

( d ) Tatu  jiiandae kuonesha   kuwa aliyekufungulia kesi alifanya hivyo bila sababu za msingi. Yaani ionekane wazi kuwa hapakuwa na sababu zozote za msingi za kufanya hivyo yaani kukufungulia mashtaka kama hayo.

( e ) Pia andaa ushahidi  au  mashahidi ili kuonesha  ni kwa kiasi gani uliathirika kutokana  na  kubambikizwa kesi ili uweze  kupata pesa ulizoomba kulipwa. Kuathirika au  kupata  madhara  kunakoongelewa hapa sio lazima ziwe athari za kimwili tu.

Zipo athari kama mtu kuharibiwa hadhi yake katika jamii, athari ya kumharibia mtu sifa njema katika jamii, na athari za kumpotezea mtu   mali pamoja na muda kutokana na kesi hiyo.

 Aidha athari ya mali na muda   inatokana na mtu kuacha kufanya shughuli zake na kuanza kusughulikia kesi hiyo ya uongo. Katika kufanya hivyo ni rahisi mtu kufukuzwa kazi au kupoteza kazi yake kwa namna yoyote ile ikiwa ni pamoja na kumharibia mtu mipango yake mbalimbali ambayo ingeweza kumwingizia kipato. Haya yote yanahesabika ni athari ambapo mtu aliyesababisha  atatakiwa  kuyafidia.

Na hizo athari si lazima  zitokee zote. Hata ikitokea moja kati ya hizi inatakiwa kufidiwa

( f ) Jambo jingine la muhimu na la mwisho katika kufungua shauri la kubambikizwa kesi ni kuwa lazima mashtaka aliyosingiziwa mtu yawe ni ya jinai. Yaani  ulisingiziwa kutenda jinai  kama kuiba, kubaka, kupiga, kutapeli, kutukana, kusingiziwa kumiliki silaha, n.k.

Imeandikwa na Bashir Yakub.
bashiryakub@ymail.com, 0784482959, 0714047241

No comments: