MKAZI wa Loksale wilaya ya Monduli, Samwel Petro Shani(47) amelalamikia hatua ya kuvunjwa mikono yake miwili kwa kipigo cha askari polisi katika kituo cha Leskale kwa madai ya kushindwa kulipa deni ya shilingi 250,000 alizokuwa akidaiwa ana mfanyabiashara wa eneo hilo.
Aidha anawatuhumi askari hao kukodiwa na mfanyabiashara mmoja mkazi wa eneo hilo kwa lengo la kumshikisha adabu baada ya mkazi huyo kushindwa kulipa deni la sh,250,000 alizokuwa akidaiwa na mfanyabiashara huyo.
Samweli ameeleza kupokea kipigo hicho ambapo alidai kuwa dhamira ya askari hao ilikuwa ni kumtoa uhai wake kwani walikuwa wakitumia chuma kinene kumpiga na kumvunja mikono yake miwili huku mwingine alikuwa akimshambulia kwa runngu na mateke.
Akizungumza kwa majonzi,Samweli alieleza kuteswa na askari hao wanaodaiwa kukodiwa na mfanyabiashara aliyemtaja kwa jina moja la bi Shamimu,ambaye alikuwa akimdai kiasi hicho cha fedha.
Alieleza kuwa tukio hilo lilitokea februali 6,mwaka huu majira ya saa 3 usiku na kwamba aliwatambua askari wawili waliomtesa kwa kipigo kuwa ni Steven na Justini wote ni askari wa kituo hicho cha Loksale.
''Mnamo tarehe 6 mwezi huu majira ya saa 3 usiku,walikuja askari wawili wakiwa wamevaa nguo za kiraia ,walinikuta nimekaa kwenye ukuta nikiwa na kijana mmoja.Walinikamata na kunifunga pingu wakiwa wamenikandamizia chini ,walinipiga sana na kunivunja mikono yangu miwili'' alisema Samweli
Akisimulia chanzo cha tukio hilo alisema ,mfanyabishara bi Shamimu alienda katika kituo hicho cha polisi na kuwaeleza askari hao kuwa alikuwa akinidai shilingi 250,000 na kwamba sikuwa nimemlipa deni hilo.
''Ni kweli Shamimu alikuwa akinidai shilingi 250,000 ila nilisha mlipa shilingi laki moja na kubaki sh,150,000 ,hizo hela kuna msichana nilimdhamini alikuwa mfanyakazi wa duka lake aliyedai alimwibia ,ndipo mimi kwa kuwa nilikuwa na mahusiano na msichana huyo nilikubali kulilipa deni hilo'' alisema Samweli
Alisema askari hao walimvamia na kumkaba kabali kisha askari mmoja alimfunga pingu na kuanza kumshambulia kwa kumpiga na rungu na chuma na walipoona wamepoteza fahamu baada ya kumvunja mikono walimkokota hadi kituo cha polisi na kuendelea kumpiga sehemu zingine za mwili ikiwemo miguuni.
''Baadae usiku wakiwa wamenifungia lokapu alikuja mkuu wa kituo na kuniangalia,alikuta hali yangu ni mbaya na kuondoka bila kusema lolote'' alisema.
Hata hivyo askari hao waliingiwa na woga kutokana na hali yake na kuamua kumchukua usiku huo wa manane na kumpeleka katika kituo cha afya kwa ajili ya matibabu.
Alieleza kuwa kesho yake askari hao walimchukua na kumpeleka kituo cha polisi wilaya ya Monduli na kumweka lokapu.
Aliongeza kuwa mkuu wa upelelezi wa wilaya OC CID,aliyemtaja kwa jina moja la bw Abichi alimfuata akiwa lokapu na kumwambia kuwa anataka ampatie dhamana ila alitakiwa akibaliane na masharti ya dhamana .
''OC CID aliniambia kuwa nataka nikupatie dhamana ila kwenye maelezo yako unatakiwa ueleze kuwa ulikuwa unatoroka ulinzi halali wa polisi ukiwa na pingu ,na wakati ukikimbia ulianguaka na pingu zikakuvunja mikono yako ''alisema bw Shani.
Aliongeza kuwa hakukubaliana na kauli hiyo ndipo oc cid alipoamua kumrudisha lokapu ,ambapo alikaa kwa muda wa siku nne wakimbembeleza akubaliane na maelezo ya polisi .
Alisema aliamua kuwa na msimamo huo hadi tarehe 12 walipoamua kumfikisha mahakama ya wilaya ambapo alisomewa shtaka la kuvunja na kuiba na kujaribu kutoroka polisi akiwa na pingu ,suala ambalo ni uongo uliolenga kupoteza haki yake ya kulalamikia jeshi hilo.
Kamanda wa polisi mkoani hapa alipotafutwa alikiri kupata malalamiko ya mkazi huyo ,hata hivyo alieleza kuwa kwa sasa yupo likizo ila aliwasiliana na mkuu wa kituo cha polisi Monduli(OCD)ili kupata undani wa tukio hilo.
Kwa upande wa mfanyabiashara ,Shamimu alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi alikana kukodisha askari wa kumpiga na kumvunja mkono mlalamikaji ila alieleza kuwa yeye alienda kituoni hapo kupeleka malalamiko yake ndipo askari hao walipoamua kumfuata mtuhumiwa na kwamba kilichotokea huko yeye hafahamu.
No comments:
Post a Comment