TAYARI imebainika kwamba, baadhi ya viongozi walioonesha nia ya kugombea urais mwaka huu wameanza kupigiwa debe na wake zao ndani ya mitandao ya kijamii ili waume hao watakapoibuka na ushindi wapate nafasi ya ‘u–First Lady’, Risasi Jumamosi linakupa zaidi!
Taarifa zilizotua juu ya dawati la gazeti hili juzi zilisema kuwa, vita ni nzito kwani baadhi ya wake wa wagombea nao wapo ndani ya mkakati wa kukusanya watu wa kuwaunga mkono waume zao katika kinyang’anyiro hicho kitakachochukua nafasi Oktoba, mwaka huu.
Wakati vita hiyo ikiwa imepamba moto, mnajimu maarufu nchini, Maalim Hassan Hussein naye ameibuka kwenye Risasi Jumamosi na kuanika utabiri mzito juu ya wasifu wa mtu atakayeshinda urais huo.
HALI ILIVYO SASA
Habari zinadai kuwa, baadhi ya wake wa viongozi hao nao wamekuwa wakipita chini kwa chini kukusanya na kuweka sawa makundi ya kisiasa tayari kwa kampeni za kuwaingiza ikulu waume zao.
ISHU NI KUMRITHI MAMA SALAMA KIKWETE
“Kila mke wa mgombea anafanya kampeni za chini kwa chini. Unajua wenyewe kila mmoja anafahamu kwamba ‘mzee’ akiingia ikulu yeye atakuwa First Lady kumrithi wa sasa (mama Salma Kikwete), ndiyo maana siku hizi karibu wake wa wagombea wote wana safari za mikoani kupanga timu ushindi,” kilisema chanzo kimoja.
FARAJA KOTA YUKO WAZI ZAIDI
Miss Tanzania 2004, Faraja Kota ambaye ni mke wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu aliyetangaza nia, amekuwa akitupia maneno yenye kumpigia kampeni mumewe huyo kwenye Instagram na mitandao mingine ya kijamii.
KWENDA NAYE KANISANI
Desemba mwaka jana, Faraja aliongozana na mumewe huyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini kwenda kwenye Kanisa la FPCT, Ilongelo na baadaye kwenye Uwanja wa Michezo wa Ilongelo, Singida ambako mumewe alitangaza rasmi nia yake ya kugombea urais.
MAMA PINDA
Tunu Pinda ni mke wa Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda. Yeye aliwahi kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema alishtushwa kusikia habari kwamba, mumewe ametangaza nia ya kugombea urais 2015.
Alisema alipomuuliza mumewe alimwambia hajaita vyombo vya habari kusema hivyo lakini muda ukifika atafanya hivyo. Mama Tunu akasema na yeye anakubaliana na maneno ya mumewe kwamba muda ukifika atangaze kugombea urais.“Kwa hiyo kama alivyosema na iwe hivyo kama Bwana Mungu aishivyo, nasema amina. Kwa sababu muda bado haujafika, utakapofika tutajua,” alisema mama Pinda.
YA MTABIRI SASA
Kuhusu utabiri wa Maalim Hassan, amesema mwaka huu, Tanzania itampata rais wa aina yake kuliko miaka yote iliyopita tangu uhuru (Desemba 9,1961).Akizungumza na gazeti hili Jumatano iliyopita, ofisini kwake, Magomeni, Dar, Maalim Hassan alisema kuwa, rais atakayepatikana mwaka huu atakuwa mtu aliyechanganya dini.
Alisema mtu huyo, kama baba yake atakuwa Muislam basi mama atakuwa Mkristo. Kama mama Muislam, baba itakuwa kinyume cha hapo.
TOFAUTI HATA KWA MKE, MUME
Maalim Hassan akaenda mbele zaidi kwa kusema: “Kama wazazi wake wote watakuwa dini moja, basi yeye (mgombea) atakuwa na imani tofauti na mke wake au mume wake (kama kutakuwa na mgombea mwanamke). “Mgombea anaweza kuwa Muislam, kama ni mwanaume basi mke wake atakuwa Muislam. Vivyo hivyo kwa mgombea mwanamke,” alisema Maalim Hassan.
KWA HARAKAHARAKA
Kauli ya Maalim Hassan ina ishara ya kumgusa moja kwa moja, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bumbuli (CCM), January Yusuf Makamba ambaye mama yake mzazi ni Mkristo huku baba yake, mzee Yusuf Makamba akiamini katika Uislam.
WANAOTAJWA KUWANIA URAIS MWAKA HUU
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitangaza nia hiyo usiku Agosti 22, mwaka jana Ikulu Ndogo ya Jiji la Mwanza.
January Makamba alitangaza nia ya kuwania nafasi hiyo Julai 2, mwaka jana alipokuwa Uingereza katika mkutano wa sekta ya mawasiliano. Wengine ni Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Khamis Andrea Kigwangallah, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Lameck Nchemba (CCM), Waziri Nyalandu (CCM), Mawaziri Wakuu Wastaafu, Frederick Tuluwai Sumaye na Edward Ngoyai Lowassa (wote CCM).
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Camillus Membe (CCM), Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Masatu Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Mganga Ngeleja (CCM). Waziri wa Uchukuzi, Samuel John Sitta naye amekuwa akitajwa kujitosa kwenye kijiti cha urais.
Kutoka vyama vya upinzani, ambaye ameshatangazwa na chama chake ni Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Peter Slaa yeye amekuwa akigombea kwa chama hicho kwa miaka kumi iliyopita. Lakini kuna tetesi kuwa, huenda Chadema ikamsimisha mwenyekiti wake wa taifa, Freeman Haikaeli Mbowe.
No comments:
Post a Comment