Kobe
wadogo 250, wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid
Amani Karume, wakiwa njiani kusafirishwa kwa njia ya magendo kwenda
Malaysia.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, alisema
kobe hao walikamatwa wakiwa wamehifadhiwa katika masanduku yaliyowekwa
maembe ndani yake, katika hatua za mwisho za kusafirishwa.
“Ni
kweli tumekamata kobe 250 wakiwa wamehifadhiwa vizuri katika masanduku
yakiwa yameingizwa maembe tayari kusafirishwa kwenda Malaysia,” alisema.
Hata
hivyo Kamanda Hamdani alikataa kumtaja mtu aliyekamatwa na kobe hao kwa
madai kwamba uchunguzi unaendelea na kitendo cha kumtaja moja kwa moja,
kinaweza kuharibu uchunguzi wa tukio hilo.
“Jeshi
la Polisi kwa sasa halipo tayari kumtaja mtuhumiwa aliyekamatwa na kobe
hao kwa sababu uchunguzi zaidi unaendelea...unajuwa ukianza kumtaja
mtuhumiwa pamoja na watu wengine, unaharibu uchunguzi mzima wa tukio
hilo,” alisema.
Katika
miaka ya hivi karibuni kumekuwa na matukio ya wizi wa kobe kutoka
Zanzibar kupelekwa sehemu nyingine duniani ikiwa ni pamoja na Tanzania
Bara.
Kobe
hao wanalindwa na sheria za kimataifa, wakiwa katika orodha ya viumbe
ambao wapo katika hatari ya kutoweka duniani, kama ilivyo kwa kasa kwa
hivyo wamekuwa katika udhibiti mkubwa.
Kwa
upande wa Zanzibar, kobe wanahifadhiwa katika kisiwa kidogo cha Chumbe
kilichopo nje ya Bandari ya Malindi umbali wa kilometa 40, ambapo hata
hivyo kumekuwepo matukio ya wizi wa mara kwa mara.
Ofisa
mmoja kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ambaye moja ya majukumu yake
ni kulinda na kuhifadhi kobe waliopo katika kisiwa kidogo cha Changuu,
alikiri kuwepo wizi katika nyakati tofauti, unaofanywa na watu
wasiokuwa waaminifu wanaotembelea kisiwa hicho kwa shughuli za utalii.
“Yapo
matukio ya wizi wa kobe katika kisiwa cha Changuu kwa nyakati tofauti,
kwani watu hufika katika kisiwa kwa shughuli tofauti ikiwemo za
matembezi ya utalii,” alisema.
Katika
miaka kumi iliyopita, zaidi ya kobe 1,500 wameibwa katika kisiwa cha
Changuu, wakiwemo kobe wadogo ambao huhifadhiwa katika sehemu maalumu.
No comments:
Post a Comment