Wanariadha kutoka nchi
jirani za Kenya na Uganda wanategemewa kuanza kuwasili mjini Moshi,
Kaskazini mwa Tanzania Ijumaa hii kwa ajili ya kushiriki mbio za
Kilimanjaro Marathon zitakazofanyika siku ya Jumapili mapema asubuhi.
Kenya
na Uganda ni miongoni mwa nchi zilizopo jirani na Tanzania ambazo
wakimbiaji wake maarufu na wanaochipukia hushiriki katika mbio hizo
zinazotambuliwa na Shirikisho la Riadha duniani (IAAF).Kuwasili mapema kwa wanariadha hao ambao idadi yao haijafahamika kwa sababu ni ya wazi (Open) ni kwa ajili ya kusoma njia zitakazotumika na kufanya usajili katika hoteli ya Keys iliyopo kati kati ya manispaa (municipal) ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mbali na Kenya na Uganda, wanariadha wengine, kwa mujibu wa waandaaji wameanza kuwasili kwa ajili ya mbio hizo, wengi wao wakiwa watalii kwa ajili ya kupata fursa ya kuuona Mlima Kilimanjaro, ambao ni mrefu kuliko milima yote barani Africa.
Zaidi ya wakimbiaji 6000 mashuhuri kutoka Kenya, Uganda na nchi nyingine za Afrika, Ulaya, America na Asia wanategemewa kuwania medali za dhahabu, Shaba na Fedha pamoja na pesa taslimu katika mbio hizo za wazi kwa raia na wageni.
Wanariadha wa Kenya walitawala mbio za mwaka jana ambapo katika mbio ndefu (full marathon-wanaume), nafasi sita za juu zilishikwa na Wakenya huku David Rutoh-akiwa namba moja na kumaliza mbio kwa muda wa 2:16:06.
Kwa upande wa wanawake (full marathon), Kenya pia ilishinda nafasi nane za juu, mshindi wa kwanza akiwa ni Fridah Lodepa akishinda kwa muda wa 2:40:26 huku Joan Rojich akimaliza wa pili katika muda wa 2:44:24
No comments:
Post a Comment