Kesi ya Mauaji ya Daudi Mwangosi : Shahidi aeleza Walivyotekeleza Agizo la Kamanda Kamuhanda - LEKULE

Breaking

13 Feb 2015

Kesi ya Mauaji ya Daudi Mwangosi : Shahidi aeleza Walivyotekeleza Agizo la Kamanda Kamuhanda



Kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Chanel ten, Daudi Mwangosi inayomkabili askari polisi, Pacificus Cleophace, jana ilianza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Iringa chini ya Jaji Paulo Kihwelo kwa shahidi wa kwanza kuelezea namna walivyotekeleza agizo la aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda. 
 
Shahidi huyo ambaye ni ofisa mstaafu wa Jeshi la Polisi katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Saidi Mnunka (61) alidai kuwa kabla ya tukio Septemba Mosi, mwaka 2012 alipata maelekezo kutoka kwa Kamanda Kamuhanda kuwa apange seksheni kwa ajili ya kuzuia ghasia siku inayofuata katika mkutano wa Chadema uliopangwa katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi.
 
Alisema seksheni hiyo ilikuwa na askari 12 aliowapatia maelekezo aliyopewa na Kamuhanda na aliwaamuru wachukue silaha kwa ajili ya kuelekea katika eneo la tukio.
 
Silaha walizochukua ni pamoja na mabomu ya machozi, virungu, mabomu ya mshindo na silaha za moto mbili.
 
Alisema wakati huo pia Serikali ilikuwa imetoa  katazo kwa vyama vyote vya siasa kutofanya mikutano ya hadhara ili kupisha kazi ya sensa ya watu na makazi iliyokuwa ikiendelea nchini.
 
 Alidai kutokana na tamko hilo, Chadema walipatiwa barua kutoka makao makuu ya Polisi Mkoa wa Iringa iliyowataka wasitishe maandamano na mkutano wao wa hadhara kama walivyokuwa wameomba.
 
Hata hivyo, alidai kuwa wafuasi na viongozi wa chama hicho walikiuka agizo la Polisi na kuamua kufanya maandamano na mkutano na walipoamriwa kutawanyika walikaidi na kuamua kuanzisha vurugu.
 
“Nilichokishuhudia siku ile niliona kikosi cha askari kikiwa kimemzunguka mwandishi wa habari huku wakimpiga, ndipo Kamanda Kamuhanda akaagiza waache kumpiga kwa kuwa alikuwa ni mwandishi, lakini kabla agizo hilo halijatekelezwa nilisikia kishindo kikubwa na nikauona mwili wa marehemu Daudi Mwangosi ukiwa umelala chini huku utumbo ukiwa nje na askari wengine wakiwa hapo chini wamejeruhiwa,” alisimulia shahidi huyo.
 
Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Sunday Ihela aliiomba mahakama hiyo ipokee gazeti la Mwananchi la Septemba 3, mwaka 2012 kama kielelezo kutokana na picha iliyokuwa imechapishwa kuhusiana na mauaji hayo.
 
Jaji Kihwelo aliiahirisha kesi ambayo inaendelea kusikilizwa leo baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Rwezaula Kaijage kupinga kupokelewa kwa kielelezo hicho akitaka mwandishi wa habari hiyo ahojiwe kwanza.

No comments: