JWTZ wapewa mafunzo kukabili majanga ya moto - LEKULE

Breaking

27 Feb 2015

JWTZ wapewa mafunzo kukabili majanga ya moto


ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kambi ya Ihumwa mjini hapa wamepatiwa mafunzo ya kukabiliana na majanga ya moto na uwezo wa kukabiliana na matukio ya moto.
 
Kutokana na mafunzo hayo sasa Jeshi hilo kupitia Kambi yake ya Ihumwa litaanza kutoa huduma za kuzima moto kutokana na kuwa na gari kwa ajili ya shughuli hiyo.
 
Hayo yalibainika jana wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya siku saba ambayo yaliendeshwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma.
 
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto, Yohana Nkunu alisema mafunzo hayo ni kwa ajili ya kupeana elimu na kuwezesha vikosi vya ulinzi na usalama katika kupambana na majanga ya moto kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi.
 
“Vitu muhimu vilivyofundishwa ni pamoja na vile vya kusaidia kudhibiti ajali za moto lengo likiwa ni kutoa elimu dhidi ya majanga ya moto na uwezo wa kukabiliana na matukio ya moto,” alisema.
 
Alisema kutokana na mafunzo hayo, jeshi hilo litasaidiana pale kunapokuwa na majanga mengine na makubwa ya kuhitaji nguvu kubwa katika kudhibiti moto.
 
Pamoja na hayo alibainisha kuwa Jeshi hilo la Zimamoto limekuwa likipata lawama mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwenye matukio lakini sababu kubwa huwa ni kuchelewa kutolewa kwa taarifa za moto unapotokea.
 
Alisema jamii bado haijawa na utayari wa viashiria vya hatari kwani mtu anaweza kuona gari linakwenda kwenye tukio likiwa limewasha taa na kupiga king’ora lakini hawezi kulipisha.

No comments: