KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, imeitaka Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kufanya ukokotoaji upya wa bei ya
mafuta ili kumsaidia mlaji wa mwisho wa bidhaa hiyo kunufaika na punguzo
la bei ya mafuta duniani.
Akiwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati hiyo, Mbunge wa
Tandahimba, Juma Njwayo (CCM) kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo
alisema utaratibu huo wa Ewura wa M-One wauangalie upya kwani unaumiza
mlaji.
Alisema
bei ya bidhaa hiyo duniani imeshuka kwa asilimia 60. Dar es Salaam
hutumia asilimia 60 ya mafuta yanayoagizwa nchini huku kampuni zinazouza
mafuta yanauza lita moja Sh 1,520 kwa jumla.
Njwayo
alisema lakini katika vituo vya rejareja Dar es Salaam bidhaa hiyo
huuzwa Sh 1,849 tofauti ya Sh 329 kwa lita moja, kwani kutokana na
kushuka kwa bei hiyo ya mafuta duniani inaweza kushuka kila mwezi.
Pia
alisema kamati inashauri serikali kwa ushirikiano na wawekezaji binafsi
kuanza ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam
kwenda mikoani ili kupunguza gharama za mafuta, usalama wa usafirishaji
pamoja na usalama wa barabara nchini.
Kamati
hiyo iliishauri serikali kuachana na mitambo ya kukodi ya kampuni ya
Songas-Gas, IPTL na Symbion kama ilivyofanya kwa Aggreko na kununua
mitambo yake kwani mitambo ya kukodi gharama yake ni kubwa.
Alisema
Tanesco iweke mpango maalumu wa muda mfupi kati na mrefu kukusanya
madeni yote wanayodai watu binafsi, serikali na taasisi zake ambazo ni
Sh bilioni 186.4 na kulipwa moja kwa moja kupitia hazina.
Akizungumzia
suala la sekta ndogo ya gesi, alisema kamati imeridhishwa na hatua za
kumalizia ujenzi wa bomba gesi na miundombinu yote ifikapo Juni, mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment