CHADEMA Yaigaragaza CCM Sumbawanga - LEKULE

Breaking

24 Feb 2015

CHADEMA Yaigaragaza CCM Sumbawanga

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeigaragaza vibaya CCM katika uchaguzi wa marudio wa Serikali za Mitaa uliofanyika jana katika kata tatu za Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Chadema ni miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na vyama vya CUF na NCCR Mageuzi.
 
Vyama hivyo viliweka makubaliano ya kushirikiana kwenye uchaguzi kwa kuachiana maeneo ambayo kuna chama kati yao kina nguvu.
 
Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana, CCM iliongoza kwa kupata jumla ya mitaa na vijiji 9,406, huku vyama vya upinzani vikigawana nafasi 3,211.
 
Uchaguzi huo wilayani Sumbawanga ulirudiwa baada ya kuahirishwa kutokana na kasoro zilizojitokeza.
 
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na msimamizi wa uchaguzi huo, Hamid Njovu, Chadema wameshinda viti 37 na CCM wakiambulia vitano tu kati ya mitaa 43 ambayo uchaguzi wake ulikuwa ukirudiwa katika kata za Msua, Chanji na Kizwite na mitaa miwili ambayo pia uchaguzi wake ulivurugika awali.
 
Njovu alisema uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti katika mtaa mmoja wa Nankasi, Kata ya Chanji, utarudiwa Jumapili baada ya kura kugongana.
 
Alisema katika Kata ya Kizwite mitaa iliyofanya uchaguzi ilikuwa 15, ambapo Chadema ilishinda mitaa 13, huku CCM wakiambulia miwili.
 
Katika Kata ya Msua, mitaa iliyofanya uchaguzi ilikuwa 13 ambapo yote ilikwenda Chadema na CCM kuambulia patupu.
Njovu alisema kwa upande wa Kata ya Chanji yenye mitaa 14, Chadema imeshinda 10, wakati CCM imepata mitatu. Mtaa mmoja uchaguzi utarudiwa.
 
Aliongeza pia uchaguzi wa marudio kwenye mitaa miwili, kila chama kiliibuka na ushindi katika mtaa mmoja, ambapo CCM ilipata ushindi Mtaa wa Bangwe, Kata ya Izia na Chadema ikishinda Mtaa wa Tambazi katika Kata ya Sumbawanga.
 
 Uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu mkubwa tofauti na ilivyokuwa awali Desemba 14 mwaka jana ambapo ulivurugika katika kata hizo kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza, ikiwa pamoja na vituo kuchelewa kufunguliwa.
 
Hali hiyo ilisababisha wananchi waliokaa vituoni kwa muda mrefu wa zaidi ya saa nane wakisubiri kupiga kura kuhamaki na kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma moto ofisi ya mtendaji wa Kata ya Kizwite na Kata ya Chanji na kuteketeza nyaraka zote muhimu za kupigia kura.
 
Hivyo kufanya mchakato mzima wa uchaguzi huo kurudiwa upya kuanzia kujiandikisha hadi upigaji wa kura.
 
Akizungumza baada ya matokeo hayo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Sumbawanga, Zeno Nkoswe, aliwashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi kupiga kura na kufanya chama chao kuibuka na ushindi wa kimbunga kiasi hicho na kudai huo ni mwanzo wa kuelekea ukombozi wa taifa hili kutoka mikononi mwa CCM ambayo inatumia vibaya rasilimali na maliasili za nchi kwa kunufaisha mafisadi.
 
Naye Katibu Mwenezi wa CCM wa wilaya hiyo, Clement Bakuli, alisema wameyapokea matokeo hayo kwa masikitiko makubwa, lakini katika mpambano wowote lazima mshindi apatikane, hivyo chama kitakaa kufanya tathmini kuona wamekosea eneo gani ili waweze kujirekebisha kwa uchaguzi ujao.
 
Timu nzima ya CCM ngazi ya wilaya ikiongozwa na mwenyekiti wake, Emmanuel Kilindu na Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hilaly, walipiga kambi na kufanya kampeni za nguvu katika kata hizo.
 
Akizungumzia matokeo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema ushindi huo ni mwelekeo wa anguko la CCM nchini.
 
“Ushindi huu mkubwa ni mwendelezo wa anguko la CCM na ni motisha kuelekea hatua ya Ukawa ya kutoshiriki kura ya maoni na badala yake kuelekeza nguvu katika kuhamasisha wananchi kuiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka huu,” alisema Mnyika.
 
Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza ratiba ya uandikishaji wapigakura ukiwamo Mkoa wa Rukwa, huku akiwataka pia wananchi kuiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
 

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema hana taarifa na matokeo hayo, hivyo hawezi kusema chochote.

No comments: