Baadhi ya wabunge wamechachamaa na kuwashukia baadhi ya mawaziri na watendaji wa serikali kwa kuzembea katika utendaji wao jambo linalosababisha upotevu wa mabilioni ya shilingi na kulisababishia taifa hasara.
Wabunge hao wameongeza pia kuwa umasikini na ugumu wa maisha kwa wananchi kwa kuongezewa kodi na tozo mbalimbali kunasababishwa na uzembe wa viongozi wachache wa serikalini.
Wakichangia mara baada ya kamati za Ardhi, Maliasili na Mazingira na ile kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji baadhi ya wabunge wamesema serikali imekuwa ikipoteza kiwango kikubwa cha fedha kutokana na uzembe huku akitolea mfano wizara ya Ardhi ambapo viwanja 260,000 vilivyotolewa hati na wizara hivi karibuni ni viwanja 22,000 pekee ndivyo vilivyopo katika kumbukumbu za wizara.
Pia zaidi ya viwanja 240,000 vikiwa havipo katika kumbukumbu za wizara na kusababisha upotevu wa kiasi cha shilingi bilioni 103 kwa mwaka wa fedha uliopita pekee na kushauri kuanzisha utoaji wa hati za ardhi kwa njia ya elektroniki kwa kushirikisha sekta binafsi.
Awali wakiwasilisha taarifa za kamati zao mwenyekiti wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira James Lembeli ametaka kufanyika kwa ukaguzi maalum juu ya matumizi ya shilingi bilioni 3.9 zilizotumika katika operesheni tokomeza.
Jambo lingine ni utekelezwaji wa maazimio ya kamati hiyo juu ya operesheni hiyo huku makamu mwenyekiti wa kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji akitaka serikali kuanza utaratibu wa kutumia mita za maji katika taasisi za uma.
No comments:
Post a Comment