Aliyewalawiti Watoto Kenya kuhukumiwa - LEKULE

Breaking

25 Feb 2015

Aliyewalawiti Watoto Kenya kuhukumiwa

Raia wa Uingereza Simon Harris, aliyedhalalisha kingono watoto waliokuwa wakirandaranda mitaani katika mji mdogo wa Gilgil nchini Kenya atahukumiwa leo nchini Uingereza.

Hii ni baada ya mahakama ya Birmingham kumpata na hatia ya kudhalalisha kingono watoto wa kiume na kupatikana na picha za utupu za watoto.

Harris mwenye umri wa miaka 55 alikuwa akiendesha mradi wa kutoa misaada kwa jamii na alikuawa mtu aliyeheshimika.

Hatahivyo alitumia nafasi hiyo kuwashawishi watoto.

Kwa takriban miaka 20 alikuwa akitumia gari lake kuzunguka katika mitaa ya Gilgil,

nia yake ikiwa kunyemelea watoto wa kiume waliokuwa wakirandaranda mitaani, kwa kisingizio kuwa alijali na kushugulikia maslahi yao.

Polisi wanasema waathirika 40 walijitokeza kutoa ushahidi.

Hatahivyo ili kufanikisha utaratibu wa mahakama ushahidi wa 11 kati yao ndiyo uliotumika.

Waathirika walitoa ushahidi katika mahakama hiyo ya Uingereza kupitia mtambo wa video uliowekwa nchini Kenya.

Mjini Gilgil nilikutana na waathirika wawili.

Vijana wenye umri wa miaka 30 ambao alimfahamu Harris wakati wakiwa na umri wa miaka 13.

Waathirika hao waliomba majina yao halisi kuhifadhiwa na kwahivyo nimewapa majina John na Allan.

John anaeleza jinsi alivyomjua Harris, ‘’ nilikua na umri wa miaka 13 wakati nilipokuja hapa mjini na kujiunga na watoto waliokuwa wakiraranda mitaani.

Walikuwa wanamfahamu Harris na kila tulipoona gari lake tulimkimbilia, alikua akitubeba na kutupeleka kwake nyumbani’’.

Naye Allan anasema umasiki mkubwa uliokuwa ukimwandama yeye na wenzake ulisababisha Haris kuweza kuwashawishi kwa urahisi,

’ kila tulipokwenda nyumbani kwa Harris ,tulijua kwamba tungepata chakula,mavazi mapya na pesa’’.

Waathirika hao wawili walikubali kuandamana name hadi alikoishi Harris.

Ni safari ya takriban kilomita 8 ,barabara yenyewe ni ya mchanga na mandhari ni ya kichani.

Nyumba yake yenye paa la kijani iliyojulikana kama ‘’The green house’’ imesimama imara juu ya mojawapo ya milima modogo ya Gilgil.
Eneo lenyewe limejitenga kwa kuwa mashamba ni makubwa na hakuna idadi kubwa ya wakaazi.

Huenda mandhari hayo yalimsaidia kuficha yaliyokuwa yakifanyika hapo.

Gari lake aina ya Land Rover ambalo alitumia kusafirisha watoto kutoka mjini limefungiwa ndani ya gereji.

John na Allan wanasema kuwa makao hayo ni kumbukumbu ya kila mara kuhusu yale waliyopitia.

''Baada ya kula chakula alikuwa akituosha bafuni, anatupatia pombe kisha anaanza kutushikashika kila mahali,asubuhi ukiamka unajikuta umelala naye kitandani’’, anasema John.

Kwake Allan hukumu dhidi ya Harris haitoshi,

‘’ ni vizuri atahukumiwa lakini serikali ya Uingereza inapaswa kutulipa fidia sisi waathiriwa kwasababu aliyotutendea yametufanya kutengwa katika jamii, hakuna anayetupenda ni vigumu sana kwetu hata kupata vibarua. Anasema.

John anaeleza jinsi jamii imekuwa ikiwachulia, ‘’wanatuchukulia vibaya sana, wengi wanadhani tulikubali kudhalilishwa kwa hiari ili tupate pesa, hawaelewi kwamba tulikuwa watoto wadogo’’.

Harris alifanya maouvu hayo wakati akiendesha mradi wa mkutoa misaada kwa jamii ambao alianzisha miaka ya 90.

Hatahivyo udhalalisha huo uligunduliwa mwaka 2013 baada ya wanafilamu kutoka Uingereza kuandaa makala iliyoangazia maisha ya watoto waliokuwa wakirandaranda mjini Gilgil.

Makala hiyo ilionyesha jinsi malalamishi ya watoto hao yalivyopuuzwa sio tu na wakaazi lakini pia maafisa wa utawala.
Afisa wa huduma za kijamii Dan Nderitu, ambaye alitoa ushahidi wakati wa kesi anasema malalamishi ya watoto hao yalipuuzwa kutokana na mtazamo wa jamii.

‘’ Watoto wa mitaani hawana sauti katika jamii, wanachukuliwa kama wanyama wa porini, hawapendwi na watu. Harris alifahamu hivyo na akatumia nafasi hiyo kuwadhalalisha kingono’’.

Waathirika wawili niliozungumza nao waliweza kupata ushauri nasaha na kubadili tabia.

Hivi sasa wanafanya kazi za vibarua kila vinapopatikana huku wakiwa na wingi wa matumaini kuwa siku moja jamii itawakubali kikamilifu.

Uchunguzi uliofanywa na serikali ya Uingereza ukasababisha kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa Simon nchini Uingereza.

Hii ni mara ya kwanza Uingereza kutumia sharia inayowezesha mahakama kufungua mashtaka dhidi ya raia wake kwa tuhuma za udhalalishaji wa kingono katika nchi ya kigeni.

No comments: