Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mkazi wa mjini Namanyere mkoa wa Rukwa, Gilbert Paul (37) aliyejiandalia maziko yake miaka 14 iliyopita, bado yu hai.
Kwa sasa mtu huyo ameanza maandalizi ya kuchimba na kujenga kaburi la gharama, ikiwa ni pamoja na kununua jeneza.
Paul, baba ya mtoto mmoja na mchoraji maarufu mjini Namanyere aliyehitimu Kidato cha Nne 2001 katika Shule ya Sekondari Nkasi, anasema anafanya hivyo kwa kuwa ana amani maisha ya duniani yana ukomo wake na ni ya kupita tu.
Aliyasema hayo juzi, akithibitisha kujichongea msalaba mkubwa na kuutundika kwenye paa la kibanda chake anamofanyia kazi zake katika Mtaa wa Sasala.
Msalaba huo mweupe mkubwa, umeandikwa tarehe aliyozaliwa ya Desemba 24, 1977, lakini katika tarehe ya kufa, ameweka alama ya kiulizo. Msalaba huo unaonekana waziwazi, kiasi cha wageni wanaopita eneo hilo, kudhani ni nyumba ya ibada.
Paul alisisitiza kuwa msalaba huo uliofikisha miaka 14 sasa, ndio utakaosimikwa katika kaburi lake, ambalo anatarajia kulichimba na kulijengea, akikadiria litamgharimu Sh milioni moja, sawa na gharama ya jeneza alilotarajia kulinunua.
“Nilipotafuta mafundi wanitengenezee msalaba huu, wote waligoma wakidai ni uchuro na hawajawahi kusikia wala kuona mtu akijifanyia maandalizi yake ya maziko akiwa bado anaishi .
“Mama alilia sana walipomtaarifu, akidai katika ukoo wa baba yangu na wa kwake hakuna aliyewahi kufanya hivyo …Baba alifariki nikiwa na miaka saba, mwanzoni watu walidhani nina tatizo la akili na wengine waliamini nimeathirika kwa Ukimwi hivyo nimekata tamaa ya kuishi, lakini sivyo…“ anasema.
Alieleza kuwa katika maisha yake yote, hakuwahi kuwa na rafiki wa kike mjini humo kutokana na kujitengenezea msalaba huo, unaomfanya wamuogope sana, hadi kuona kuna ulazima wa yeye kwenda kijiji cha mbali na hapo .
“Nilichumbia na kuoa chapuchapu nikihofia mke wangu mtarajiwa akibaini nimejitengenezea msalaba hatanikubali,“ alieleza.
Mke wa Paul, Paskaria Salvatory (25) akizungumzia tukio hilo, anasema kama angefahamu, kamwe asingekubali kuolewa naye.
“Si kawaida mtu kujitayarishia maziko yake mwenyewe akiwa hai. Nilibaini mwezi mmoja baada ya kuolewa, kwa kweli nilishituka sana, pia wanawake wenzangu walikuwa wakinibeza na kuniita kwa majina ya kuudhi, lakini sasa nimezoea na nimezaa naye mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili. Mume wangu ana akili timamu, ni mwenye huruma na anayejali familia“, alibainisha.
No comments:
Post a Comment