Afisa Elimu Mbinga avuliwa madaraka - LEKULE

Breaking

3 Feb 2015

Afisa Elimu Mbinga avuliwa madaraka



BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma limemvua madaraka afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Daniel Mkali baada ya kufanyiwa uchunguzi kwa muda kwa tuhuma mbalimbali zilizotajwa na baadhi ya madiwani pamoja na viongozi wa idara hiyo ya elimu msingi na kuelekea kutishia kuibuka kwa mgogoro wilayani humo.
Akitangaza uamuzi huo wa kumvua wadhifa huo pamoja na kumshusha cheo na kutakiwa kupangiwa shule ya kufundisha mwenyekiti wa halmashauri hiyo ya Mbinga Alanus Ngahi, mbele ya madiwani pamoja na watumishi wengine wa halmashauri hiyo amesema uamuzi huo umefikiwa na kamati ya maadili iliyokutana kujadili suala hilo la kinidhamu na kiutumishi na baraza hilo kuridhia hatua zichukuliwe dhidi ya afisa elimu huyo.
Akizitaja tuhuma nne zilizokuwa zikimkabili afisa elimu huyo, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Hussein Isa amesema ni pamoja na kusajili asasi isiyokuwa ya kiserikali iliyojulikana kwa jina la (UWEKAMBI) umoja wa waratibu elimu kata ya Mbinga na kuwaagiza walimu wakuu wa shule za msingi wilayani humo kuhamishia fedha zote za capitation na michango ya Umitashumta jumla ya shilingi milioni 232 ambapo katika fedha hizo shilingi milioni 60 ni michango ya Umitashumta, milioni 10 ni michango ya wazazi na shilingi milioni 61 ni fedha kwa ajili ya capitation na mitihani zilipelekwa kwenye akaunti yenye namba 61714000405 iliyopo katika benki ya NMB tawi la Mbinga.
Ameitaja tuhuma nyingine kuwa ni kughushi nyaraka kwa lengo la kutoa fedha kupitia ununuzi wa mafuta ya diesel lita 5500 na petrol lita 5500 na kuwaagiza walimu wakuu wachangie fedha za kupiga picha wanafunzi wa darasa la saba pamoja na fedha kwa ajili ya TSM 9 kwa maelekezo hayo ni kosa kwa sababu alikuwa akijua kuwa gharama za TSM 9 hugharamiwa na serikali kwa asilimia mia moja.
Amesema kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 12.47 zilipelekwa kwenye akaunti hiyo ya UWEKAMBI na ameitaja tuhuma nyingine kuwa ni kumdanganya mwajiri kuwa hakujakusanywa fedha yoyote kutoka kwa wazazi na hakuna fedha ya capitation iliyopelekwa kwenye akaunti hiyo ya UWEKAMBI.
Aidha mkurugenzi mtendaji amesema baada ya maamuzi hayo yaliyotolewa na baraza la madiwani hatua nyingine zinazohusishwa na mamlaka nyingine zikiwemo za kinidhamu zitafuata ingawa kwa sasa anapaswa kuyatumikia maamuzi yaliyotolewa na baraza hilo la madiwani.

No comments: