Tume ya Kuzuia Rushwa nchini Sierra
Leone, ACC imewaamuru watu 40 kufika katika ofisi zake kufuatia ukaguzi
wa ndani uliofanyika ambao umetuhumu kwamba mamilioni ya dola ya fedha
iliyopangwa kutumika katika kupambana na ugonjwa wa Ebola, haijatolewa
maelezo. Imekuja siku chache baada ya ripoti ya ukaguzi kutolewa
ikituhumu kuwepo vitendo vya udanganyifu katika kusimamia fedha za nchi
kuhusu ugonjwa wa Ebola.
Mwandishi wa BBC kutoka mji mkuu wa
Sierra Leone, Freetown, Umaru Fofana amesema ripoti inawajumuisha
maafisa wandamizi kutoka wizara ya afya, wafanyabiashara na wanaharakati
wa vyama vya kijamii ambao ripoti hiyo imedai kuwa walipokea fedha kwa
ajili kutumia katika kampeni dhidi ya ugonjwa wa Ebola.Mkuu wa ACC, Joseph Kamara ameiambia BBC kuwa watu hao 40 ni sehemu tu ya idadi kubwa ya watu wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa nchini Sierra Leone akisema wameanzia chini kupanda juu katika uchunguzi wao.
Amesema kundi lifuatalo litaitwa na ofisi yake mara baada ya watuhumiwa wa sasa kuchunguzwa na kushitakiwa pale unapopatikana ushahidi wa kutosha. Amri hiyo imekuja baada ya chama tawala cha All People's Congress kutoa wito wa kuzuiwa kusafiri nje kwa watu wote waliotajwa katika ripoti hiyo. Katika siku zilizopita watu walioaminika na Tume ya Kuzia Rushwa kuwa na kesi ya kujibu walinyang'anywa hati zao za kusafiria na waliachiliwa kwa dhamana hata kabla ya kesi dhidi yao kuanza rasmi kusikilizwa na mahakama.
Ripoti hiyo imewasilishwa mbele ya bunge la nchi hiyo kujadiliwa.
No comments:
Post a Comment