Wizi wa Kupindukia....Kamati ya Zitto Kabwe Yafichua namna Mabilioni ya Fedha yanavyoibiwa Serikali - LEKULE

Breaking

30 Jan 2015

Wizi wa Kupindukia....Kamati ya Zitto Kabwe Yafichua namna Mabilioni ya Fedha yanavyoibiwa Serikali



TAARIFA ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ya hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu na mashirika ya umma kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2013, imebua wizi wa kutisha wa fedha za umma uliofanywa na taasisi hizo.
Hayo yalibainika jana wakati Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo, ambapo alisema katika ripoti za ukaguzi kwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), imebainika kuwa ililipa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ndege iliyoikodi kutoka Shirika la Ndege la Wallis Trading Inc la China, ndege ambayo ni hewa kwa kuwa haipo nchini.
“Hadi sasa Serikali imelipa dola za Marekani 26,115,428.75, (Sh bilioni 45.17) na sasa inadaiwa dola za Marekani 23,996,327.82 (Sh bilioni 41.51), ndege hiyo ilikuwa mbovu na ilifanya kazi nchini kwa miezi sita pekee badala ya miaka sita kama mkataba wa ubinafsishwaji ulivyotaka,” alisema Zitto katika taarifa yake.
Taarifa hiyo ya PAC, ilibainisha pia kuwa katika ujenzi wa jengo la watu mashuhuri (VIP) katika Uwanja Ndege wa Kimatifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, kuna ufisadi wa takriban Sh bilioni tisa.
Ilisema pia jengo hilo lilianza kujengwa bila kibali cha Baraza la Mawaziri na kuwa thamani ya gharama za ujenzi wa jengo hilo hazijulikani kwa kuwa nyaraka muhimu hazipo.
Kwa upande wa Mamlaka ya Bandari (TPA), imebainika kutumia Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya vikao vya wafanyakazi na mamilioni mengine kujilipa kwa ajili ya posho za safari bila kuwa na kibali kutoka serikalini.
Zitto alisema pia kamati yake imebaini kuwa misamaha ya kodi imezidi kuongezeka na kufikia Sh trilioni 1.8 mwaka 2014, huku zaidi ya Sh bilioni 80.45 za misamaha hiyo kwa mwaka zikitumika kwa njia zisizo halali.
“Mbali na hilo, pia fedha za pembejeo za kilimo zimekuwa zikitumika visivyo halali na kwa zao la korosho, zaidi ya Sh bilioni moja zilitumika kinyume cha taratibu,” alisema Zitto.
Kwa upande mwingine, ripoti hiyo imesema mifuko ya hifadhi ya jamii ipo hoi kutokana na Serikali kushindwa kulipa deni la Sh trilioni 1.87 ilizokopa.
Pamoja na hilo, taarifa ya PAC imesema pia Serikali ina hatihati katika hisa zake zilizopo katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), endapo hatua za kulipa deni la Sh bilioni 22 hazitachukuliwa hadi kufikia Machi 31.

No comments: