WAHUDUMU wanaofanya kazi katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wamegoma kuzika miili ya watu iliyoharibika na isiyotambuliwa kwa madai kuwa hawajalipwa mishahara yao kwa kipindi cha miezi sita.
Tarifa ya kugoma kwa wahudumu hao imekuja baada ya kuwapo kwa maiti ambazo hadi sasa imeshindikana kuzikwa.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, wahudumu hao tisa, walisema tangu Juni mwaka jana hadi sasa hawajalipwa mishahara yao licha ya kufikisha madai yao katika uongozi wa hospitali hiyo na halmashauri.
Wahudumu hao ambao wameajiriwa kwa ajira za muda (vibarua) wametangaza kutofanya kazi ya kuzika maiti ambazo hutakiwa kuzikwa na halmashauri kutokana na kutolipwa kwa malimbikizo yao.
Walisema katika madai yao, wanaidai hospitali hiyo zaidi ya Sh milioni 2 huku wakibainisha kuwa kila mmoja anadai Sh 260,000 kwa ajili ya malipo ya kazi wanayofanya ya maziko.
“Kwa kawaida sisi ambao tunafanya kazi ya kuzika maiti ambazo hutakiwa kuzikwa na halmashauri kama imeshindakana kutambulika, huwa tunalipwa Sh 10, 000 kila tunapofanya kazi ya kuzika, lakini kwa muda wa miezi sita hatujawahi kulipwa licha ya kuwa tunafanya kazi hiyo kila
mara,” alisema Maduhu Girya.
Wakati wahudumu hao wakichukua uamuzi huo, kuna maiti iliyokaa kwa siku nane mochwari bila kuzikwa, huku mwili ambao umeshindwa kutambuliwa na ndugu na jamaa zake unatakiwa kukaa katika chumba hicho kwa muda wa siku tatu hadi nne ambapo baada ya hapo hufanyiwa uchunguzi kisha kuzikwa.
“Hadi sasa ni siku nane huo mwili haujatolewa mochwari sababu kubwa tumegoma kuzika, kama harufu itakuwapo sisi hatujali, tunataka kwanza tulipwe haki yetu,” alisema John Samson.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Godfrey Mpangala, alikiri kuwapo kwa madai ya wahudumu hao na mgomo huo ambapo alibainisha kuwa tatizo lilitokana na Serikali kutopeleka fedha za matumizi mengine, hivyo kushindwa kuwalipa.
No comments:
Post a Comment