Taifa linaugua ebola ya kisiasa - LEKULE

Breaking

2 Jan 2015

Taifa linaugua ebola ya kisiasa

SITOKUWA nafichua siri yoyote nisemapo kwamba taifa la Tanzania linaelekea pabaya; kwamba limefisidiwa na linaendelea kufisidiwa na wenye kulifisidi ni viongozi wake. Walewale waliokula amini kulilinda taifa na kulitumikia ndio walewale walio safu ya mbele kulichimba, kuliaibisha na walio tayari kulitosa.

Siyasemi haya kwa mzaha. Nayasema kwa uchungu kwa sababu hakuna asiyejuwa kwamba viongozi hawa wakiachiwa waendelee kufanya wayafanyayo wataiangamiza Tanzania. Kwa hali ilivyo ni kama kwamba taifa zima limo katika hali ya hatari. Ni hali yenye kutisha.

Chenye kutisha zaidi ni kwamba uroho wa viongozi hao unaifanya hata hali ya usalama wa taifa iwe hatarini. Ni jambo jepesi kabisa kwa viongozi wa sampuli hii kuiuza nchi yao. Tena wanaweza wakaiuza kwa bei ya kutupwa;kwabei “mrakhas” kama tusemavyo mitaani Unguja.

Wananchi wasipokuwa macho wanaweza wakafanyiwa kiini macho wakaja ghafla kushtukia kuwa taifa silao tena, tayari limekwishapigwa mnada. Hawana tena na chao;si leo wala uchao.

Hii ndiyo hatari inayoikabili Tanzania yenye viongozi walio waroho, wasiolifikiria taifa.Ukichunguza kwa makini utaweza kutambua kwa nini ikawa ni viongozi haohao walio vifua mbele kuikataa Rasimu ya Katiba iliyotungwa kwa kuyazingatia mapendekezo ya wananchi.

Peleleza zaidi na utang’amua kwa nini wanashikilia mfumo wa Muungano uwe wa serikali mbili na si serikali tatu.

Misimamo yao yote hiyo inafungamana. Kuitupilia mbali Katiba ya wananchi kutawawezesha waendelee kulifisidi taifa. Hilo ni jambo lililo dhahiri kabisa.

Viongozi hawa wasio na mvuto wa kisiasa wamelifanya taifa nalo lisiwe tena na uzito wake wa kisiasa uliokuwa nao kwa muda wa kama miaka 20 au hata 25 baada ya uhuru — sio tu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki lakini katika bara zima la Afrika.

Nimesema, na nitasema tena kwamba juu ya taksiri zake, Julius Nyerere aliifanya nchi iheshimike na viongozi wake wajiheshimu. Hii leo Tanzania haina tena ile heshima iliyokuwa nayo katika miaka ambapo ikipigiwa mfano kwa namna ilivyokuwa ikijitahidi kuonyesha kwamba viongozi wake wanaongoza kwa uadilifu.  Na si Nyerere tu bali hata na mawaziri wake na wakuu wengine wa serikali.

Zama hizo nchi iliyokuwa ikinuka kwa ufisadi katika ukanda wa Afrika ya Mashariki ilikuwa ni Kenya. Leo mambo yamegeuka.Tanzania iliyokuwa safi juu ya umasikini wake sasa imeipita Kenya kwa jinsi inavyonuka ufisadi.

Si kwamba Kenya imetakasika na haina tena ufisadi. La. Imejaa tele ufisadi uliopenya katika kila sehemu ya dola lakini taasisi za kimataifa zinazoyapima mambo haya ya ufisadi yanatwambia kwamba Tanzania ina ufisadi uliokithiri kuupita ule wa Kenya.

Kuna jambo moja adhimu ambalo Nyerere alilifanya alipokuwa anajenga misingi ya taifa huru baada ya madhila ya ukoloni, madhila ambayo wengi wa Watanzania waleo wanayasikia tu. Nyerere aliuokoa utu wa mwananchi.

Baada ya uhuru na alipokuwa anatafakari ni njia gani ya kuifuata kulipatia taifa maendeleo Nyerere alihoji kuwa ni kheri kuwa na utu kuliko kuwa na kitu. Hiyo haikuwa hoja nyepesi.Ilikuwa ni hoja nzito iliyojaa hikma na uadilifu.

Nakiri kuwa hoja hiyo inaweza kuwa na utata.Huenda isishangiliwe na wengi hususani katika enzi hizi za  uroho na utapiamlo.

Huenda ikawa hivyo kwa sababu viongozi wa leo wamekuwa wakiwapa wananchi darsa mpya wakitumia kisingizio cha sera za ulibirali mamboleo. Kwa matendo yao wanawafunza wayapende waliyokuwa wakiyachukia na wayachukie waliyokuwa wakiyapenda.

Hiyo ndiyo hali ilivyo siku hizi.Tanzania ina viongozi wenye mori wa kuyaheshimu matumbo yao tu. Miradi wanayoisimamia kwa dhati ni miradi yao binafsi. Badala ya kuijenga nchi wanajijenga wenyewe. Wanapojijenga wanakuwa wanazidi kuibomoa imani ya wananchi.

Viongozi hao wanafanya wayafanyayo wakitambua kwamba hakuna litalowafika, kwamba ingawa sheria ina macho lakini itawafumbia macho. Na wala mkono wake hautowafikia. Wanajuwa hali ni hiyo kwa sababu wanalindana.

Matokeo ya yote hayo ni kwamba taifa limekuwa halina mawalii wala malaika katika ngazi za juu za uongozi. Huko unakutana na mijizi na mijangili hata wakiwa wamesoma kufika mbinguni na hata wakiwa na mashahada kwapani mwao.Tena ni majingili wasio na upeo na wenye uongozi usiosisimua.

Hii leo hata mtoto wa skuli anajuwa nini Richmond, nini Akaunti ya Tegeta Escrow au nini maana ya kuichakachua Katiba mpya.Anajuwa nini maana ya madudu hayo na nini athari zake, ingawa huenda ufahamu wake ukawa wa juujuu tu.

Tangu ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL ianze kujadiliwa Bungeni Watanzania wamezidi kufahamu namna viongozi wao wanavyolindana. Wamefahamu jengine pia kwamba baadhi ya wafanya biashara wakubwa wanashirikiana na baadhi ya vigogo serikalini katika mitandao isiyo tofauti na ile ya majambazi wa kimafia wenye chimbuko lao huko Sicily, Italia. Mbinu wanazozitumia ni zilezile zikiwa pamoja na vitisho na mauaji.

Mbinu hizo za Kimafia zitazidi kutumika nchini Tanzania miezi ijayo hasa kukaribia uchaguzi mkuu kwani sasa tunaambiwa hatukuona kitu bado. Kazi ya kuufichua ufisadi inaendelea na Januari au Februari mwakani tutayasikia ya viroja kuhusu kashfa nne nyingine.

Kati ya hizo kubwa inahusika na vibali vya kuagiza na kuingiza sukari nchini. Tutawajuwa wenye kuvihujumu viwanda vya sukari nchini kwa kuagiza sukari kutoka nje wakishirikiana na viongozi fulani serikalini. Hujuma hizo zinaweza zikaviua viwanda vya kuzalisha sukari nchini.

Halafu kuna matokeo ya uchunguzi uliofanywa juu ya mikataba ya gesi walioandikiana wakuu fulani wa serikali na makampuni ya gesi.

Isitoshe kuna ripoti ya uchunguzi juu ya kubinafsishwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) pamoja  na ripoti maalum juu ya Bandari ya Dar es Salaam.Haya ya Bandari si madogo.

Mtu anaweza kutengeneza filamu nzima ya kusisimua kuhusu kashfa za Bandari ya Dar es Salaam. Wahusika ni mawaziri, wakuu wengine wa serikali, wawekezaji kutoka nje na mabilioni kwa mabilioni ya shilingi.

Ninaamini kuwa tukiitathmini historia ya Tanzania tutaona kuwa hakuna wakati ilipokuwa na viongozi wepesi, wasiojuwa wafanyalo ili kuyanyanyua maisha ya wananchi kama hawa tulionao sasa — tena kote Bara na Zanzibar. Pengine unaweza kuhoji kwamba maadili ya Tanzania yalianza kuporomoka tangu alipong’atuka Nyerere baada ya sera zake za kiuchumi kushindikana na watu walipoanza kughilibiwa na mfumo wa uchumi wa ulibirali mamboleo.

Jambo la kushangaza na lenye kutisha ni kuwa hawa viongozi wa leo wanawashajiisha wananchi wa kawaida wawe upande wao. Wanajigeuza sura kwa kujifanya kuwa wao ndio wazalendo halisi. Wanalifanya taifa kuwa ni lao wao tu, ni milki yao na kwamba wao ndio taifa na taifa ndio wao.

Hiyo ni ishara ya watu walio majnuni. Ndio maana mara kwa mara tunawasikia baadhi ya viongozi hao wakitoa matamshi ya kimajnuni.

Utamaduni wa kisiasa wa Tanzania umeambukizwa na ugonjwa hatari. Hatari yake ni kwamba unaweza kuwa ugonjwa usiosikia dawa. Hii ebola ya kisiasa imeiathiri mihimili yote ya dola: Ikulu, bunge na mahakama. Yote imeguswa na maradhi hayo, hakuna iliyonusurika.

Wakati mwingine unakaa na kujiuliza iwapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina mtu mwenye kuiendesha na kuiongoza au inajiendea yenyewe tu? Bila ya dira na bila ya kujuwa wapi inapotaka kwenda.

Nchi yenye mtu mwenye kuiongoza haiwezi kuwa inajienda hivi kiholelaholela, haiwezi kuwa kama chura ikawa inachupachupa kutoka kashfa moja hadi nyingine.

Pengine utajiuliza Watanzania wanaweza kuirekebisha nchi yao? Jawabu ni kwamba wanaweza. Swali linaloweza kulifuatia hilo ni wafanye nini ili waweze kuirekebisha?

Nadhani hatua yao ya mwanzo wanaweza kuichukuwa Oktoba ijayo wakati wa uchaguzi mkuu kwa kuzipiga kura zao kwa busara. Huu sio tena wakati wa kutumia hamasa za kichama kwa maamuzi nyeti kama hayo ya uchaguzi.

Viongozi wenye nakisi ya uadilifu hawafai.Hamna hili wala lile. Waondolewe kwenye madaraka na washtakiwe. Katika nchi yenye viongozi wenye kulindana kazi hiyo ni kazi ya wananchi. Silaha yao ni kura zao. Wazitumie kuisafisha jamii.Hii ni dhima iliyowaangukia Watanzania wote.

No comments: