Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ndugu wananchi;
Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha usalama wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa salama.
Uhalifu Unapungua
Ndugu Wananchi;
Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia wema. Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Ajali za Barabarani
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048 zilizosababisha vifo vya watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383 zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali 8,335, vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao hawajakamatwa.
Ndugu wananchi;
Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Ndugu wananchi;
Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikilinganishwa na ndovu 219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaani Tanzania Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na mapambano dhidi ya ujangili.
Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori zitaendelezwa kwa nguvu zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na mali katika mapambano haya. Naomba waendelee kutusaidia.
Hali ya Uchumi Jumla
Ndugu wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia au hata kuvuka lengo tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Hali nzuri ya upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya mfumuko wa bei kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Mauzo Nje
Ndugu Wananchi;
Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia Oktoba 31, 2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,503.9 ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi kama bei za kahawa, chai, korosho na pamba zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo isingepada.
Akiba ya Fedha za Kigeni
Ndugu Wananchi;
Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,251.8 kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi 4.1. Hii ni chini ya lengo letu la kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu. Hata hivyo, sina wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali zilizosababisha lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha makusanyo yafikie lengo na ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu ya kwanza.
Takwimu Mpya za Pato la Taifa
Ndugu wananchi,
Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote duniani kuwa na mwaka unaotumika kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato la Taifa. Ni utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka wa kizio hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika marekebisho hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na huduma mpya katika pato la taifa na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa picha halisi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka 2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya marekebisho ya takwimu zao za pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka huu (2014). Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la taifa. Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu wananchi;
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato la taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka 2007. Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 53.17. Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila Mtanzania kutoka shilingi 1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za mwaka 2001 hadi shilingi 1,560,050 (sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo na Chakula
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini. Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni 14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25. Katika ziada hiyo, mahindi yanachangia tani milioni 1.55, mchele tani 794,000 na kiasi kinachobakia kinachangiwa na mazao mengine ya chakula.
Ndugu wananchi;
Kuna jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo ningependa kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama wote unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu ya nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba ya taifa ya chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana na uwezo wa maghala yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhi tani 246,000 ingawaje tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi tani 400,000 ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani 292,415.41 mwaka huu ina maana kwamba kiasi cha karibu tani 50,000 zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo utaratibu mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa siku moja.
Ndugu wananchi;
Baada ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tani milioni 2.96 za nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya kuuza mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna budi kulitafutia majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani na hata nje ya nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa chini na kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili lenye maslahi makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa jumla.
Ndugu Wananchi;
Katika mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao kufanikisha azma yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao wajitokeze kufanya biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo.
Miradi ya Kimkakati
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) umeendelea vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka 2015 miradi mingi itakamilika.
Tuanze na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015. Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza lengo letu la kuzalisha MW 2,780 za umeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini umeendelea vizuri na tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano wake katika historia ya nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014, jumla ya vijiji 3,836 vimepatiwa umeme na vingine 1,500 vinategemewa kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na asilimia 43 ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watu milioni 2.3 sawa na asilimia 7 walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka na kuwa milioni 7.4 sawa na asilimia 21. Haya ni mafanikio makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi kifupi kiasi hiki. Ni mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu katika kuinua hali za maisha ya Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba siku si nyingi kutoka sasa, makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga yataweza kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa. Maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme, ujenzi wa mgodi wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha chuma.
Natoa pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua iliyofikiwa. Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira 33,000 za moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu Wananchi;
Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la Kiuchumi (Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings International na Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu mingine itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.
Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote nchini. Huu nao ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19 zenye urefu wa kilometa 1,459 zimekamilika kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Morogoro, Arusha, Tabora na Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara nyingine 24 katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu, Katavi, Tabora, Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati wo wote mwaka 2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara nyingine nane yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.
Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu Mfuko huo umetengewa shilingi bilioni 751.7 ukilinganisha na shilingi bilioni 504.4 mwaka jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo na Daraja la Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la Malagarasi ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu pia kwamba mabasi yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Halikadhalika, tunategemea katika mwaka 2015 ujenzi utaanza wa barabara zinazozunguka jiji la Dar es Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine (flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile, daraja jipya la Salenda litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria 300 cha MV Dar es Salaam kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam Kaskazini na Ferry mapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Usafiri wa Anga na Reli
Ndugu wananchi;
Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea kwa mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa 274 ya mzigo yamenunuliwa. Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya Januari na Mei, 2015 tunatarajia kupokea vichwa vipya vya treni 13. Uboreshaji huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi katika reli hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye uwezo wa kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi zaidi, juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi kujenga zinaendelea. Wakati huo huo, tunaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya TAZARA ili mambo yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa Zambia. Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga mkono juhudi zetu za kufufua reli ya TAZARA.
Usafiri wa Anga
Ndugu Wananchi;
Sekta ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya abiria wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini imeongezeka kutoka abiria milioni 2.5 mwaka 2013 hadi abiria milioni 3.5 kufikia Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje zimeongezeka kutoka 274 Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba, 2014. Hili ni ongezeko la asilimia 8. Safari za ndege ndani ya nchi nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458 mwaka 2013 hadi safari 241,922 mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 39. Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na biashara nchini zimeendelea kukua.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3) la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri. Jengo hilo litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa abiria milioni 8 kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2 (Terminal 2) utafanyika ili liweze kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi huo, Wakala wa Viwanja vya Ndege wameendelea kukarabati na kuboresha viwanja vya ndege vya KIA, Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora na Kigoma. Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga kuanza mapema mwaka 2015.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini. Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu 36,339 kati ya 81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu 45,223 yaani 26,946 wa shule za msingi na 18,277 wa shule za sekondari hususan wa masomo ya sayansi. Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari.
Mwaka huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi 5,602 wa masomo hayo wamedahiliwa. Mpango huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa tulilonalo la walimu wa sayansi katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi wa Maabara
Ndugu wananchi;
Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za Kata 3,463 umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688 sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara 494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Ndugu Wananchi;
Natoa pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja na wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada hizo, nimeongeza miezi sita zaidi kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo. Naomba watumie kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali itasaidia upatikanaji wa watunza maabara (laboratory technicians) ambao tumeanza programu kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.
Ununuzi wa Vitabu
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabu milioni 2.5 vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari. Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili. Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo mwaka 2016.
Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Ndugu wananchi;
Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya elimu nchini hakuna badala yake. Sera mpya inalenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora na inayolinga na wakati tulionao. Jambo jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kuanza kutafakari namna jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue iliyowapata watu 1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati yao. Kwa upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege vya kimataifa na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema kuwahudumia wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.
Mwaka huu pia, Madaktari wetu watano wamekwenda Liberia kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Madaktari wetu hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari hao watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya taifa katika kupanga mipango ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine katika kutibu wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu Wananchi;
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa sekta ya afya 8,345 ambao kati yao kuna madaktari 244, madaktari bingwa 75, wauguzi 2,555 na wataalamu wa kada nyingine za afya 5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 7,956 katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730. Kwa ongezeko hilo, sasa tumefikia asilimia 97 ya lengo letu la kudahili wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017.
Jitihada zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na wataalamu wengine wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya kufundishia pale Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi huo ukikamilika Chuo kikuu cha Muhimbili kitaweza kudahili wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa sasa jambo ambalo litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Afya kupata jawabu la uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo na mishipa ambalo limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata vifaa.
Maji
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili hiyo miradi 498 ya maji vijijini imekamilika na miradi 740 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 378 ipo katika maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba katika mwaka ujao wa 2015, miradi mingine 731 itatekelezwa na vituo 25,790 vya kuchota maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza kuwafikia asilimia 71 ya wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 58 ya sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la kuwapatia watu maji asilimia 65 ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu kwa ndugu zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu zaidi na wawapatie fedha kwa wakati.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga – Same – Mkomazi pamoja na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza ameshapatikana. Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana muda si mrefu kutoka sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa mji wa Orkesment.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na tatizo la upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji kadhaa ambayo miradi imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote mwakani itakamilika. Jiji la Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka Serikali ya India imefikia hatua nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.
Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 268.2 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora, Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji ya Sikonge na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge na Mahakama
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza vyema majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamoja na kulazimika kugawana Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge limefanya mikutano mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano na maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya msingi 569 na ya nyongeza 1,541yaliulizwa na kujibiwa. Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo lilijadiliwa na kutolewa maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu maazimio hayo na bado tunaendelea.
Napenda kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa kutekeleza vizuri wajibu wao wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema na chanya kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa ya kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote. Wahenga wamesema “mcheza kwao hutunzwa”. Hatuna budi kutoa pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kwa uongozi wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea malengo ya kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua 200 kwa mwaka kila mmoja wao.
Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri. Mashauri 870 yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Rufani, mashauri 11,334 kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715 kwenye Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika Mahakama za Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga na Tabora umesaidia sana kupunguza mrundikano wa mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea mashauri mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika historia ya Mahakama nchini.
Ndugu Wananchi;
Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote kwa kazi nzuri waifanyayo.
Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wote wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji Mahakamani umebadilika na kuwa bora zaidi. Mimi naahidi kuendelea kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa kwa wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea bila ya ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237 na wamekamilisha uchunguzi wa mashauri 545. Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni 428. Mashauri yaliyomalizika ni 205, kati ya hayo 125 watuhumiwa waliachiliwa na 80 walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi bilioni 38.96 zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji, maafisa wapya 394 wameajiriwa.
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kwa heshima inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014 na zilifanyika sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana sana. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa nusu karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni mafanikio makubwa. Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini Muungano wetu utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani yale mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Miaka 50 ya JWTZ
Ndugu Wananchi;
Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na taasisi muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1 Septemba, 1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani Arusha.
Nilibahatika kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na kiwango cha utayari kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri mkubwa, ujasiri, ukakamavu na uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita. Niliwapongeza siku ile na narudia tena leo kuwapongeza. Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na Watanzania wote kuwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile tunalolijua sisi sote, lakini limezidi lile lililomng’oa mvamizi Dikteta Iddi Amin wa Uganda, tena limezidi kwa mbali.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote, mchakato uliozaa Katiba Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi yake kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8 Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa kuchapisha katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30 Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi kufanya matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.
Ndugu Wananchi;
Moja ya mambo muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Register. Uandikishaji wa majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata katika Majimbo ya Mlele, Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia kuboresha mfumo huo kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye sifa stahiki kuanza.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa mfumo mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa Daftari la Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo walikuwa wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale waliopoteza vitambulisho vyao. Safari hii wanaandikishwa wote wapya na wa zamani na wote watapata vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye vitambulisho vya kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze kujiandikisha wakati ukifika.
Jambo la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftari hilo hilo litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo basi, kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu utajinyima fursa ya kushiriki kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako, Mbunge wako na Diwani wako. Katu usikubali yakukose hayo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni wajibu wa viongozi hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha uchaguzi ni wakati mzuri wa kufanya tathmini ili wapate mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya kuimarisha mazuri na kusahihisha makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani watambue matatizo ya kiusalama yaliyotokea na kuona namna ya kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo yasijitokeze tena. Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika kutekeleza malengo na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika, tunategemewa kuongoza katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya vikao vya Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu ambayo utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi cha uongozi wetu.
Kwa niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi kuwa hatutawaangusha. Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu na wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi kuwa wabunifu kwa nia ya kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa matunda ya maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda tuliyoyatarajia tulipoamua kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC, AU NA UN
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mashirika haya ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wa SADC tutaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ile ya kisiasa na kiusalama kama ilivyoainishwa katika RISDP (Regional Indicative Strategic Development Plan) na SIPO (SADC Strategic Indicative Plan for the Organ). Kwa ajili hiyo Tanzania, itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza utangamano wa kiuchumi katika SADC na kusaidia kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa na kusalama kati ya nchi wanachama.
Kwa upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu wa Umoja wa Afrika na kuchangia katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa Mataifa tutaendelea kutimiza wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa kimataifa ulio adhimu na muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi wetu katika majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa watatutaka tufanye hivyo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Namaliza hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja wetu na mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka 2015 kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu. Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu. Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment